• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 6:50 AM
Ukuzaji avokado wageuka hatari kwa sababu ya donge nono

Ukuzaji avokado wageuka hatari kwa sababu ya donge nono

NA RICHARD MAOSI

MSIMU wa kuvuna kwa wakulima kutoka eneo la Kinangop katika Kaunti ya Nyandarua umegeuka wakati wa kilio kwa sababu ya wizi wa maparachichi.

Soko la maparachichi, au avokado, limepanuka ulimwenguni hali inayofanya wengi kunufaika kutokana na uuzaji wa mazao.

Lakini baraka hii ya soko kupanuka imealika makateli na magenge ya wahalifu wanaolenga kuiba mazao ya wakulima ambapo hata wale walioko vijijini hawajasazwa.

Jambo ambalo limewasukuma baadhi ya wakulima kufuga mbwa wakali, kuwasaidia kushika doria nyakati za usiku.

Kwa mujibu wa baadhi ya wakulima Kinangop, wezi wanatoka katika maeneo jirani ya Ndonyo Njeru, Ol-Kalou, Naivasha, Dundori, na Nakuru.

Mzee Kenneth Muraya kutoka Kinangop aliambia Taifa Jumapili kuwa kilimobiashara cha avokado kimekuwa hatari kwa sababu baadhi ya wakulima wamekuwa wakishambuliwa wanapokuwa wakiwekea mashamba yao ulinzi.

Kulingana na Mzee Muraya, msimu wa kuvuna kila mwaka huwa ni baina ya Februari na Aprili.

Anasema mwaka 2023 aliajiri mlinzi wa usiku ila aliamua kuacha kazi baada ya wezi kumzidia nguvu jioni moja akiwa katika harakati ya kulinda mazao.

Anasema amejaribu mbinu mbalimbali kama vile kuweka uzio wa seng’enge kuhakikisha anawakabili wezi lakini wapi!

Hivi sasa Mzee Muraya analenga kuweka waya wa umeme ili kuwakomesha kabisa wahalifu hao ambao wamekuwa wakimsababishia hasara kila ifikapo msimu wa kuvuna.

Bi Alice Wangare naye anasema avokado hufanya vyema katika Kaunti ya Nyandarua kwa sababu ya kiwango cha juu cha mvua, inayoshuhudiwa kila mwaka.

Isitoshe bei yake huwa ni nzuri sokoni.

“Kutoka kwenye mti mmoja wa spishi ya avocado ya hass, mkulima anaweza kulipa kodi na karo ya watoto wake kwa mwaka mzima,” akasema Bi Wangare.

Malalamiko yako pia kwingineko.

Hali ni kama hiyo katika eneo la Ziwa Kaunti ya Uasin-Gishu ambapo wakulima wengi, kwa kuchoshwa na wizi wa kila mara, wameanza kuwazia namna ya kuachana na kilimo cha parachichi na kuweka zingatia kwa kilimo cha aina nyingine.

Siku chache zilizopita, wakulima kutoka Kaunti ya Murang’a waliweka mikakati ya kulinda maparachichi baada ya kubainika wezi walikuwa wameongezeka sana.

Soko kubwa la maparachichi kutoka Kenya liko bara Uropa, Marekani na bara Asia.

Kenya ilipiku Afrika Kusini katika uuzaji wa zao la parachichi nje ya nchi.

Maparachichi kadhaa yakiwa yameshavunwa tayari kupelekwa sokoni. PICHA | RICHARD MAOSI
  • Tags

You can share this post!

Mgombea wa urais FKF ahofia maisha yake ushindani ukitiwa...

Wapangaji nyumba za Martha wafutiwa kodi ya Januari

T L