Ulipuaji wa jengo na utekaji nyara Kiunga mpakani Somalia watia hofu
ULIPUAJI wa jengo mjini Kiunga, katika mpaka wa Kenya na Somalia, Kaunti ya Lamu, Ijumaa iliyopita, umefichua mfululizo wa matukio ya kuhofisha yanayohusishwa na operesheni za kupambana na ugaidi.
Imebainika kuwa, mwendo wa saa moja jioni ya Alhamisi, mwanamke anayemiliki jengo hilo ambako alikuwa anaishi na kuendesha duka la jumla, alichukuliwa pamoja na watoto wake na watu wanaoaminika kuwa polisi.
Ulipuaji ulifanyika karibu saa moja unusu usiku wa kuamkia Ijumaa, na familia hiyo ikaachiliwa huru saa tisa usiku, saa chache tu baada ya shambulio.
Cha kushangaza, mapema jioni hiyo serikali ya Uingereza ilikuwa imetoa upya onyo lake la usafiri dhidi ya Kenya, ikiwatahadharisha raia wake “kutoenda kabisa katika maeneo ya mashariki ya Kenya, yakiwemo maeneo ya mpaka na Somalia”.
Maeneo haya yanajumuisha sehemu za Kaunti za Lamu, Garissa, Wajir na Mandera zinazopakana na Somalia.
Duru katika ngazi za juu za usalama zilisema kuwa, jengo lililolipuliwa lilikuwa linafuatiliwa kwa karibu. Afisa aliyeomba kutotajwa jina kwa sababu ya uzito wa suala hilo, alisema ilishukiwa kuwa, baadhi ya bidhaa katika duka hilo zilikuwa zikitumiwa kusaidia shughuli za kigaidi, na watu waliokuwa wakilitembelea mara kwa mara waliaminika kuwa wafuasi wa Al-Shabaab.
Akizungumzia tukio hilo, Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki George Kubai, alijaribu kutuliza hofu za wananchi bila kulihusisha moja kwa moja na shambulio la kigaidi.
“Maafisa wetu, wakiwemo polisi na jeshi, tayari wapo eneo la tukio kubaini kilichotokea. Kwa sasa, wananchi wasiwe na wasiwasi. Tushirikiane na vyombo vyetu vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia katika uchunguzi ili wahusika wakamatwe na kushtakiwa,” alisema.
Mnamo Desemba 2021, duka jingine lilishambuliwa kwa vilipuzi na watu wasiojulikana saa nane usiku.
Katika matukio yote mawili, hakuna vifo au uporaji wa mali, hasa vyakula ambao hushuhudiwa wakati wa mashambulio ya kigaidi katika eneo hilo ulitokea.
Ulipuaji wa Ijumaa ulitokea wiki mbili tu baada ya mfanyabiashara mwingine kutoweka kwa njia ya kutatanisha.
Familia ya Bw Mohamed Obo, 41, ilisema alikuwa amesafiri hadi Kiunga mwezi uliopita kutatua matatizo yanayohusu mashua yake aliyokuwa amekodishia mwenzake.
Akiwa Kiunga, alianzisha makao ya muda ana aliendelea na biashara yake, akinunua samaki kutoka kwa wavuvi wa eneo hilo na kuwasafirisha kuwauzia wafanyabiashara wengine kisiwani Lamu.
Kaka yake, Bw Ali Omar, alifichua kwamba mwezi uliopita mfanyabiashara huyo aliitwa na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) mjini Kiunga.
Kulingana na Bw Omar, ilidaiwa kwamba, tangu kaka yake afike Kiunga, matukio ya utovu wa usalama yalianza kushuhudiwa katika mji huo.
Familia hiyo ilikanusha madai yanayomuhusisha ndugu yao na ukosefu wa usalama, ikiamini ilikuwa ni njama iliyopangwa na wapinzani wake wa kibiashara.
“Kaka yangu hivi majuzi alikuwa amebadilisha bei ya samaki anayonunua kutoka kwa wavuvi, kutoka Sh120 ya awali hadi Sh150 kwa kilo. Huenda jambo hili liliwaudhi washindani wake wakaamua kumchongea kwa wanausalama,” alisema.
Mkewe, Bi Tima Hassan, alisema wanaume wenye miraba minne waliwavamia nyumbani wakiwa na silaha.
Walimpiga rafikiye Bw na kumwangusha chini kisha naye akafungiwa chumbani, wakaenda na mumewe mahali kusikojulikana.
Naibu Kamishna wa Lamu Mashariki, Bw Kubai alithibitisha kisa hicho kiliripotiwa lakini akasema polisi hawakuhusika.
Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la Haki Africa, Bw Yusuf Aboubakar, alimpa Inspekta Jenerali wa Polisi, Bw Douglas Kanja makataa ya siku saba kufichua kwa umma aliko Bw Obo la sivyo ashtakiwe mahakamani.