Habari za Kitaifa

Unashambulia Bunge ilhali ni wewe umelifanya mali binafsi? Wakosoaji wachemkia Ruto

Na DOMINIC OMONDI August 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto majuzi aliwashambulia wabunge akidai wao huitisha hongo kutoka kwa maafisa wakuu wa serikali wanaofika mbele ya kamati zao.

“Wabunge wetu sharti waonywe. Wanaitisha pesa kutoka kwa maafisa wa serikali kuu, mawaziri na magavana, hasa wale ambao hufika mbele yao kuwajibikia masuala mbalimbali,” akasema alipofungua rasmi Kongamano la Ugatuzi la 2025 mjini Homa Bay.

Kauli ya Rais ilishtua wengi kwa sababu ilifichua ukweli ambao husemwa kwa minong’ono kwamba Bunge ni kitovu cha ufisadi.

Hata hivyo, wakosoaji wanasema kuwa Rais mwenyewe na serikali zilizotangulia, mara nyingi zimekuwa zikihujumu uhuru wa Bunge. Tawala hizo zilihakikisha kuwa Bunge linazingatia matakwa yao wala sio kuikosoa Serikali Kuu.

Mfano ni mnamo 2023 kabla ya wabunge kupiga kura kuhusu Mswada wa Fedha ulioanzisha Ushuru wa Nyumba.

Baada ya kung’amua kuwa mswada huo ulikabiliwa na upinzani, Rais Ruto alitoa kauli iliyofasiriwa kama vitisho kwa wabunge.

“Ninasubiri kuona wabunge watakaopinga mpango wa serikali wa kutoa nafasi za ajira kwa vijana wetu, wengi wao wakiwa wapigakura wao,” Rais akasema akiwa Narok.

Ujumbe ulikuwa wazi kwamba wale ambao wangethubutu kupinga mswada huo wangeadhibiwa.

Presha kama hiyo kutoka kwa Serikali hudhoofisha wajibu wa Bunge kama wawakilishi wa raia katika mchakato wa utungaji sheria na hata utayarishaji wa bajeti.

“Katiba hii ililirejeshea Bunge la Kenya mamlaka yake katika ugavi wa mapato, utayarishaji bajeti na kupiga msasa matumizi ya pesa za serikali, mamlaka ambayo ilipokonywa wakati wa enzi za utawala wa kiimla wa Rais Daniel Moi,” akasema wakili na mchanganuzi wa masuala ya uongozi Javas Bigambo.

Kulingana na mtaalamu huyo, Bunge la Kenya limefanya kazi nzuri katika ugavi wa fedha kwa serikali za magatuzi.

Lakini wachanganuzi wanasema itakuwa vigumu kwa mtu kupata mafanikio mengine ya Bunge la Kenya ndani ya miaka 15 iliyopita.

Kulingana na kipengele cha 95 Bunge lina wajibu wa kubaini kiwango cha ugavi wa fedha kati ya Serikali ya Kitaifa na Serikali za Kaunti huku likifuatilia matumizi ya fedha hizo.

Kipengele cha 221 kinalipa Bunge mamlaka ya kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi yanayowasilishwa na Serikali Kuu.