Habari za Kitaifa

Unaweza kufa ukidai serikali ikikupa kandarasi  

Na COLLINS OMULO March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANAKANDARASI ambao walifanya ukarabati katika Jumba la Kimataifa la Mikutano (KICC) kwa kima cha Sh1.9 bilioni bado wanadai serikali Sh350 milioni, miaka miwili baada ya kumaliza mradi huo.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KICC James Mwaura amesema kuwa bado wanasubiri deni hilo lilipwe na Hazina ya Kuvumisha Utalii (TPF) ambayo iligharamia ukarabati huo.

Akiongea mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano ya Bunge la Seneti, Bw Mwaura alishikilia kuwa ukarabati huo uligharimu Sh1.9 bilioni.

Hii ni kinyume na madai kuwa gharama ya mradi huo ulizidishwa na Sh3.2 bilioni zikatumika.

“Gharama ya kukarabati KICC ilikuwa Sh1.98 bilioni na pesa hizo zilitoka Hazina ya Kuvumisha Utalii. Bado tunapokea pesa kutokana hazina hiyo kulipa deni na Sh350 milioni ndizo tunadaiwa,” akasema Bw Mwaura.

Mwaka jana, wabunge walianzisha uchunguzi kuhusu madai kuwa serikali ilitumia Sh3.2 bilioni kukarabati KICC licha ya kuwa Sh1.9 bilioni ndizo ziliidhinishwa na Bunge.

Ukarabati huo ulifanyika kuelekea Kongamano la Afrika Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi mnamo Septemba 2023.

Bw Mwaura alisema ukarabati huo ulishirikisha jumba zima na vyumba vya mikutano, kumbi za mikutano na maua yaliyopandwa kurembesha mandhari ya KICC.

Hata hivyo, utata ulikumba mradi huo huku wanakandarasi 14 wakilalamika kuwa wanadai Sh674.6 milioni licha ya kuwa walimaliza asilimia 80 ya kazi ambayo ilifuatiliwa na jeshi, KDF.

Wizara ya Ulinzi ilitengewa Sh1.25 bilioni kulipa mwanakandarasi mkuu ambayo ilikuwa kampuni ya WY Yi kutoka China.

Kando na KICC, wanakandarasi ambao wamekuwa wakiihudumia serikali ya kaunti na serikali kuu wamekuwa wakilalamikia madeni kubwa ambayo wanadai baada ya kumaliza kazi.

Kufikia Septemba 2024, serikali ya kitaifa ilikuwa ikidaiwa zaidi ya Sh528 bilioni na wawasilishaji bidhaa pamoja na kampuni zilizopewa kandarasi kutekeleza miradi mbalimbali. Kiwango hicho sasa kimeongezeka na kufika Sh664.7 bilioni.

Mashirika ya serikali ndiyo yana deni kubwa ambalo ni Sh410 bilioni huku wizara na idara za serikali zikiwa hazijalipa Sh118 bilioni.

Katika kile ambacho kitawaumiza wawasilishaji bidhaa zaidi, kamati iliyokuwa ikiongozwa na aliyekuwa Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Edward Ouko ilizua maswali kuhusu deni la Sh268 bilioni ambalo serikali kuu inadaiwa.

Hii ni kwa sababu ya kukosekana kwa stakabadhi zinazohitajika kuonyesha jinsi ambavyo deni hilo lilivyokuja.