Upasuaji wabaini risasi tatu kati ya tano zilikwama mwili wa Ong’ondo Were
UCHUNGUZI wa maiti uliofanyiwa mwili wa Mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were Jumatatu ulionyesha kuwa alipigwa risasi mara tano huku risasi tatu zikisalia mwilini mwake.
Haya yalifanyika wakati washukiwa wa wanne wa mauaji hayo Williamn Imoli Shighali, Juma Ali Haikai, Douglas Muchiri Wambugu na David Mihigo Kagame ambao walihusishwa na mauti ya mbunge huyo, wakifikishwa katika Mahakama ya JKIA.
Shighali, Haikai na Kagame walikamatwa pamoja wakiwa Roysambu jijini Nairobi. Polisi walipewa siku 30 kuwazuilia washukiwa hao kwenye vituo vya polisi vya Ruaraka, Muthaiga, Capitol Hill na Kilimani huku uchunguzi ukiendelea kuhusu mauaji hayo.
Kortini wachunguzi walifichua kuwa wanafahamu pikipiki iliyotumika kumfuata mbunge huyo kutoka majengo ya bunge, barabara ya Wabera kisha mzunguko wa Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Nairobi ambako alipigwa risasi na kuuawa.
Jana Mwanapatholijia Mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor alifichua kilichomuua Bw Were baada ya kufanyia mwili wake upasuaji wa muda wa saa mbili.
“Marehemu mbunge alipigwa risasi mara tano na risasi mbili zililenga bega lake la kushoto huku nyingine ikitoka na moja ikikwama,” akasema Dkt Oduor.
Wachunguzi wanaamini kwamba aidha aliinua mkono wake kujilinda ama alikuwa akiongea kwa simu alipovamiwa. Ripoti ya Dkt Oduor pia ilisema risasi nyingine mbili zilimpata kwa kifua, moja ikitoka na nyingine ikikwama
“Risasi ilipenya hadi kwenye moyo, mapafu, ini na aota. Risasi nyingine ilimpata kwenye mgongo upande wa juu na kubakia ndani. Marehemu hangenusurika na aliaga kutokana na majeraha mabaya ya viungo vya mwili,” akaongeza Dkt Oduor.
Alifafanua kuwa mwili wa Bw Were haukuwa na majeraha yoyote kando na yale yaliyotokana na risasi alizopigwa na aliyemvamia mnamo Aprili 30.
Bw Were atazikwa Ijumaa kwenye kijiji cha Kachien, Kasipul, Homa Bay. Mwili wake utasafirishwa kwa ndege Alhamisi baada ya ibada Nairobi.