Habari za Kitaifa

Urafiki wa Ndindi Nyoro na Ruto waisha baada ya kuchezewa rafu

Na WAANDISHI WETU March 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

URAFIKI wa kisiasa ambao ulinawiri kati ya Rais William Ruto na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kabla, wakati wa kampeni na baada ya Kenya Kwanza kuingia mamlakani ulionekana kufikia kikomo rasmi jana mbunge huyo alipopokonywa wadhifa alioshikilia Bungeni.

Bw Nyoro alivuliwa uenyenyekiti wa Kamati yenye ushawishi ya Bajeti na Ugavi (BAC) ya Bunge la Kitaifa, huku harakati za kuwaondoa wabunge wanaomuunga mkono aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kutoka uongozi wa kamati za Bunge zikichukua mkondo mpya.

Kufikia wakati mchakato wa kumuondoa Gachagua ulianzishwa mwaka jana, Bw Nyoro na Rais Ruto walikuwa marafiki na hata wakati mmoja jina la mbunge huyo lilitajwa miongoni mwa waliofikiriwa kurithi Gachagua kama naibu rais.

Urafiki huo uliingia doa, Bw Nyoro alipokosa kutangaza msimamo wake katika kuondolewa kwa Gachagua na akakosa kufika bungeni kupiga kura.

Rais Ruto alipounda serikali Jumuishi baada ya kuanza ukuruba na kiongozi wa ODM Raila Odinga, mbunge huyo alianza kulengwa kuondolewa huku washirika wa rais katika Kenya Kwanza wakimshambulia vikali hadi jana alipovuliwa wadhifa alioshikilia kwa miaka miwili ukatwikwa mbunge wa Alego Usonga Samuel Atandi wa ODM.

Mabadiliko katika BAC yameifanya kuwa mara ya kwanza tangu katiba mpya ilipoanza kutumika mwaka wa 2010 kwa mbunge asiye wa chama au muungano tawala kuongoza kamati hii muhimu inayoshirikiana na serikali katika kupanga sera za kifedha za nchi.

Uchaguzi wa Bw Atandi, kumrithi Bw Nyoro ulifanywa kwa kauli moja. Nyoro alikuwa ameiongoza kamati hiyo kwa miaka miwili na nusu.

Mabadiliko haya yalifuatia mpango uliopangwa kwa umakini kati ya muungano wa Kenya Kwanza na ODM, ambao uliwaondoa wabunge washirika wa Gachagua kutoka uongozi wa kamati za Bunge.

“Nashukuru Serikali Jumuishi kwa kuniamini kuongoza kamati hii muhimu. Naahidi kufanya kila niwezalo kuhakikisha mgao wa rasilimali za taifa unafanyika kwa haki, usawa, na uwazi,” alisema Bw Atandi katika hotuba yake ya kukubali uteuzi.

Bw Nyoro alikuwa mmoja wa washirika wa karibu sana wa Rais Ruto baada ya Kenya Kwanza kushika madaraka, na jina lake lilitajwa miongoni mwa wale walioweza kuwa wagombea wenza wa urais katika uchaguzi wa 2027.

Hata hivyo, umaarufu wake ulianza kufifia baada ya kutochukua msimamo thabiti kuhusu hoja ya kumng’oa Gachagua madarakani. Mpaka sasa, Nyoro bado anashikilia msimamo huo wa kati.

Kanuni za Kudumu za Bunge la Kitaifa, chini ya kifungu cha 178, zinatoa mwongozo wa uongozi wa kamati za Bunge. Kamati za idara mbalimbali huchagua wenyeviti na manaibu wao kutoka miongoni mwa wanachama wao.

Hii ina maana kuwa mwanachama yeyote wa kamati husika, awe kutoka chama tawala au la, anaweza kuwa mwenyekiti au naibu mwenyekiti wa kamati hizo.

Hata hivyo, Kanuni hizo zinaweka masharti maalum kuhusu nani anaweza kuongoza au kuwa naibu wa Kamati ya Uhasibu wa Umma (PAC), Kamati ya Uwekezaji wa Umma (PIC) na Kamati ya Utekelezaji (CoI).

Katika mabadiliko mengine ya uongozi wa kamati, wabunge washirika wa Gachagua waliopoteza nyadhifa zao ni pamoja na Gathoni Wamuchomba (Githunguri), aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Katiba (CIOC), na Wanjiku Muhia (Kipipiri), aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu wa Kanda.

Bi Wamuchomba amehamishiwa kwenye Kamati ya Huduma na Vifaa vya Wabunge, ambayo haina ushawishi mkubwa, huku nafasi yake ikichukuliwa na Mbunge wa Runyenjes, Eric Karemba, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kazi, huku Mbunge wa Tiaty, William Kamket, akiteuliwa kuwa naibu wake.

Bi Muhia amebadilishwa na Mbunge mteule Irene Mayaka.

Pia, Mbunge wa Embakasi, James Gakuya, mshirika wa karibu wa Gachagua, ameondolewa kutoka uenyekiti wa Kamati ya Biashara, Viwanda na Ushirika. Anatarajiwa kubadilishwa na Mbunge wa Ikolomani, Bernard Shinali hii leo

Bw Gakuya amepelekwa Kamati ya Utangazaji wa Bunge na Maktaba, ambayo inakaa vikao mara chache, hivyo haimpi fursa ya kujipatia marupurupu mengi kama kamati zingine.

Mbunge wa Kilifi Kusini, Ken Chonga, alichaguliwa kuongoza Kamati ya Kazi.

Mnamo Machi 11, 2025, Bunge lilimkosoa Bw Nyoro na wanachama wa BAC kwa kupendelea maeneobunge yao katika mgao wa rasilimali.

Wanachama wa BAC walimtaka Bw Atandi kuhakikisha usawa na uwazi katika ugavi wa bajeti ya kitaifa.

“Uko na kibarua. Masuala ya ugavi wa rasilimali kwa usawa yamekuwa na utata. Tumekuwa tukikosolewa na Bunge,’ alisema Mbunge wa Kitui ya Kati, Makali Mulu, ambaye ndiye mwanachama wa muda mrefu zaidi wa BAC.

“Lazima tuunde mfumo wa kufuatilia miradi kote nchini, na utashangaa kuona kuwa wale waliotukosoa vikali ndani ya Bunge ndio waliopata manufaa makubwa zaidi,” aliongeza Bw Mulu, akimrejelea Kiongozi wa Wengi Bungeni, Kimani Ichung’wah (Mbunge wa Kikuyu), mshirika wa rais ambaye alimshambulia vikali kwa Bw Nyoro.