Usajili wa kidijitaji waja kufagia wafanyakazi hewa
Kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) mnamo Jumanne, waziri Kuria aliungama kuwa kuna idadi kubwa ya wafanyakazi hewa serikalini, hali ambayo inachangia serikali kupoteza pesa nyingi kupitia ulipaji wa mishahara na marupurupu mbalimbali.
“Hii ndio maana serikali, kupitia kwa Wizara ya Utumishi wa Umma ina mpango wa kufanya usajili upya, kwa njia ya kidijitali ili kunakili watumishi wote wa umma wanaolipwa kwa pesa za mlipaushuru. Kando na hayo, wizara yangu itaendesha ukaguzi wa kina wa orodha ya watumishi wa umma katika kila Wizara, Idara na mashirika ya serikali. Watumishi hao ni pamoja na walimu na maafisa wa vikosi mbalimbali vya usalama,” Bw Kuria akaeleza.
“Ni kinaya kwamba Kenya ni nchi ya watu ambao ni waumini wa madhehebu mbalimbali, lakini haijafaulu katika kutokomeza mapepo au mizimwi. Nchi hii imejaa mizimwi. Tunawalipa walimu na wafanyakazi hewa. Tunatumia pesa nyingi kwa wanafunzi hewa. Tunatuma pesa nyingi kwa wakongwe ambao hawapo,” Bw Kuria akaandika.
Alisema ni sharti mambo kulainishwa.
“Huku tukiendelea kuondoa mapepo, Wizara ya Utumishi wa Umma itaanzisha mpango wa usajili mpya wa kidijitali wa sisi wote watumishi wa umma 900,000 tunaolipwa kwa pesa za walipa ushuru, wakiwemo wale wanaohudumu katika serikali za kaunti. Ukaguzi wa orodha ya wafanyakazi wanaolipwa mishahara pia utafanywa,” Bw Kuria akaeleza.
Tangazo la Bw Kuria linajiri wiki tatu baada ya uchunguzi ulioendeshwa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) ndani ya miaka 10 iliyopita, kubaini kuwa jumla ya wafanyakazi 2,064 waliajiriwa kwa kuwasilisha stakabadhi feki za masomo na kitaaluma.
Aidha, wiki iliyopita Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) Nancy Macharia aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) kwamba tume hiyo ilitumia kitita cha Sh460 milioni kulipa mishahara kwa walimu hewa.
Ni baada ya ufichuzi huo ambapo Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Maalum John Mbadi iliamuru afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu kuendesha ukaguzi wa kina kubaini chanzo cha dosari hiyo ili “pesa hizo zikombolewe.”