Ushauri wa Ida Odinga wakati wa sherehe ya ‘Raila Birthday’ ulivyotuliza dhoruba ODM
MAMA Ida Odinga Jumatano aliingilia mzozo wa ndani unaoendelea kutokota ndani ya Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), akihimiza makundi yanayokinzana kujiepusha na makabiliano ya hadharani na badala yake kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo.
Haya yanajiri huku maafisa wakuu wa chama wakikiri kuwa migawanyiko hiyo inaendelea kudhoofisha mshikamano wa ODM kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Mama Ida alitoa wito huo wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya miaka 81 ya Raila Odinga zilizofanyika katika makazi yake ya Karen, Nairobi.
Alionya kuwa vita ndani ya chama vinaweza kudhoofisha hadhi ya ODM kama chama cha kitaifa.
“ODM lazima ibaki imara na yenye umoja ili kuwahudumia Wakenya,” alisema, akiongeza kuwa mshikamano ndani ya chama ni nguzo muhimu ya urithi wa kisiasa wa Raila pamoja na misingi ambayo ODM ilijengwa juu yake.
Alirejelea pia mtindo wa uongozi wa Raila kama mfano wa kuigwa katika kutatua migawanyiko ya sasa ya chama, akisema, “Baba aliendesha ODM kwa kujitolea. Alikiongoza kwa uthabiti na haki. Aliongoza kwa misingi thabiti. Aliendesha chama kwa mashauriano ya mara kwa mara na kwa kuwarejelea wananchi.”
Kauli yake inajiri wakati ambapo mvutano unaongezeka kati ya makundi yanayoshindana ndani ya chama, ukichochewa na tofauti kuhusu uongozi, mikakati ya kisiasa na uhusiano wa ODM na serikali ya Kenya Kwanza.
Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, alikiri kuwepo kwa misukosuko hiyo lakini akasisitiza kuwa chama bado kiko imara.
Alikubali kuwa tofauti za ndani haziwezi kukosekana katika harakati kubwa za kisiasa, lakini akasema ODM imeweka mifumo ya kushughulikia migogoro bila kudhoofisha chama.