Habari za Kitaifa

Ushauri wa wakuu wa jeshi, NIS waudhi raia

Na BENSON MATHEKA March 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wanaendelea kutoa hisia zao kufuatia kauli tata za Mkuu wa Majeshi (CDF) Jenerali Charles Kahariri na Mkurugenzi wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), Noordin Haji, kuwaonya raia dhidi ya tamko maarufu la ‘Ruto must Go’ (Ruto lazima aende).

Wanasiasa, viongozi wa mashirika ya kijamii, wanafunzi na watumiaji wa mitandao ya kijamii wameshtumu wawili hao kwa kauli zao wakisema zinakadamiza uhuru wa kujieleza.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kiongozi wa Chama cha People’s Liberation Party Martha Karua, na Seneta wa Busia Okiya Omtatah, wamekashifu maafisa hao wa usalama kwa kile wanachosema ni kuingilia siasa na kutishia uhuru wa kidemokrasia wa Kenya.

Akizungumza katika hafla ya kanisa huko Naivasha jana, Gachagua alimshauri Jenerali Kahariri kutojihusisha na masuala ya siasa. “Ningependa kumwambia CDF Kahariri kuwa jeshi linaheshimiwa sana katika nchi hii kwa sababu limekuwa likifanya kazi yake kitaaluma tangu uhuru. Tafadhali msichanganye siasa na masuala ya kijeshi,” alisema Gachagua.

Alisema kazi ya jeshi ni kulinda taifa dhidi ya vitisho vya nje na sio kushiriki mijadala ya kisiasa. Pia alifafanua kuwa kauli ya ‘ Ruto lazima aende ‘ si wito wa mapinduzi bali ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa 2027.

|”Kauli hii ni wito wa maandalizi ya uchaguzi ujao. Wananchi wanajiandaa kwa kura ya kumtoa Ruto madarakani kwa mujibu wa Katiba,” alisisitiza Gachagua.

Kwa upande wake, Martha Karua alitaja kauli ya Kahariri kama ukiukaji wa Katiba, akisisitiza kuwa jeshi halifai kuegemea mrengo wowote wa kisiasa. “Ni jambo la kusikitisha kuona mkuu wa majeshi akijitosa kwenye siasa na kujaribu kuelekeza wananchi kuhusu uhuru wao wa kutoa maoni,” alisema Karua.

Alisema kauli za Kahariri na Haji zinaonekana kama jaribio la kuzima upinzani na kuwatia hofu wananchi. “Serikali inapaswa kusikiliza kilio cha wananchi badala ya kutumia idara za usalama kuwanyamazisha. Wito wa ‘Ruto lazima aende’ ni ujumbe wa kisiasa ambao serikali inapaswa kushughulikia badala ya kujaribu kutumia vitisho kuuzima,”alisema Karua.

Seneta wa Busia Okiya Omtatah naye alitaka uchunguzi wa Bunge kuanzishwa dhidi ya madai ya matumizi mabaya ya idara za usalama kwa malengo ya kisiasa.

Alisema Kenya ni taifa la kidemokrasia, na idara za usalama hazipaswi kutumika kisiasa kumlinda au kumuondoa kiongozi yeyote. “Sheria iko wazi. Katiba ya Kenya inasema idara za usalama hazipaswi kujiingiza kwenye siasa. Jeshi linapaswa kuzingatia majukumu yake ya kikatiba na si kushiriki mijadala ya kisiasa,” alisema Omtatah.

Alionya kuwa historia ya Afrika inaonyesha madhara ya wanajeshi kuingilia siasa, akitaja mifano ya mapinduzi yaliyosababisha machafuko na migogoro katika mataifa mengine.

“Tumejifunza kutoka kwa historia kwamba kushiriki kwa jeshi katika siasa huleta udikteta, kudorora kwa uchumi na ukandamizaji wa raia. Hatutakubali hilo Kenya,” alisisitiza Omtatah.

Pia aliwataka Jenerali Kahariri na Noordin Haji kutoa tamko la hadharani kueleza misimamo yao kuhusu kushiriki kwa jeshi katika siasa.Mvutano huu umejiri wakati ambapo maandamano na migomo dhidi ya utawala wa Rais Ruto imeendelea kuongezeka.Katika miezi ya hivi karibuni, kauli ya ‘ Ruto lazima aende’ imekuwa wimbo wa wananchi katika mikutano ya hadhara, makanisa, vilabu vya burudani, na hata mechi za kimataifa.