Ushuru mpya kuumiza wenye mapato ya chini
WAKENYA wataendelea kuvumilia hali ngumu ya maisha katika mwaka wa kifedha ujao baada ua kutozwa ushuru mkubwa wa bidhaa na huduma huku serikali ikilenga kupata pesa za kufadhili bajeti yake ya Sh4 trilioni na kulipa madeni.
Kwa sasa, deni la Kenya ni Sh10.3 trilioni na ili kulilipa, serikali inapanga kutoza ushuru bidhaa za kimsingi ambazo hazikuwa zikitozwa ushuru na kuongeza baadhi ya ushuru ambao imekuwa ikitoza Wakenya.
Waziri wa Fedha Profesa Njuguna Ndung’u anapendekeza msururu wa hatua za ushuru zikiwemo kuongeza ushuru wa bidhaa za nguo zinazoingizwa nchini kwa asilimia 35 hatua inayomaanisha bei ya nguo za mitumba zinazotumiwa na Wakenya wengi wa mapato ya chini itapanda.
Hii ni pamoja na kutoza ushuru wa ziada wa thamani wa asilimia 16 kwa bidhaa za kimsingi ambazo hazikuwa zikitozwa ushuru kama njia ya kuongeza mapato.
Serikali inapanga kukopa Sh597 bilioni kujaza pengo katika bajeti, hatua ambayo itaongezea Wakenya mzigo wa madeni.
Waziri Ndung’u alisema ili kujaza pengo la bajeti, serikali itakopa Sh263 bilioni kutoka mashirika ya kifedha humu nchini na Sh333 bilioni kutoka nje ya nchi.
Katika mwaka wa kifedha unaokamilika Juni 30, serikali haikutimiza lengo lake la kukusanya mapato ya Sh360 bilioni kupitia ushuru ambapo ushuru wa VAT ulichangia kiasi kikubwa cha mapato.
Profesa Ndung’u alianzisha ushuru wa asilimia 2.5 wa magari kila mwaka ambao unatarajiwa kupitishwa kwa mlipa ushuru kupitia huduma za uchukuzi wa abiria na bidhaa.
Wakulima wataathiriwa na bajeti ya serikali ya mwaka huu ambayo imefungua milango ya kuingizwa kwa mayai, viazi na vitunguu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki bila kutozwa ushuru.
Japo hatua hii itafanya bei ya bidhaa hizo kupungua, wakulima wa humu nchini watapata hasara kufuatia ushindani kutoka kwa wenzao.
Huku serikali ikipanga kuanzisha ushuru wa asilimia 2.75 kufadhili mpango wa afya kwa jamii (SHIF), bajeti ya wizara ya Afya imepunguzwa kwa Sh14 bilioni kutoka Sh 141 bilioni hadi Sh127 bilioni.
Bidhaa za chuma na mabati zinatozwa ushuru wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 ilivyo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hii itafanya gharama ya ujenzi kuongezeka. Jana, kinara mwenza wa Azimio Martha Karua aliwataka Wabunge kuokoa raia kwa kukataa Mswada wa Fedha wa 2024.
Kulingana na Bi Karua, Mswada waFedha wa 2024 utaumiza raia zaidi iwapo Bunge halitaufanyia marekebisho.
“Swali letu ni je, utawala wa Ruto na Bunge utasikiliza kilio cha wananchi kuhusiana na mswada huu. Hakuna uhalali kutoza ushuru wa ziada kwa watu ambao tayari wamelemewa,” Bi Karua alisema.
Kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi alishutumu utawala wa Rais William Ruto kwa kuwaadhibu Wakenya kwa kukopa na kuwabebesha mzigo wa ushuru.
“Tumeshindwa kuishi kulingana na uwezo wetu. Unakopa na kuongeza ushuru. Serikali hii inatenda mabaya kuliko iliyopita,” Bw Wandayi alisema.
Wadadisi wanasema hatua za ushuru zinatokana na masharti makali ya Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF).