Habari za Kitaifa

Ushuru unaotozwa kondomu, mojawapo ya sababu za matumizi yake kupungua Kenya  

Na LINET AWOKO September 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MATUMIZI ya mipira ya kondomu yamepungua nchini ndani ya miongo miwili iliyopita, kulingana na data iliyotolewa kwenye ripoti kuhusu hali ya Afya Ulimwenguni.

Kulingana na ripoti hiyo, maarufu kama Global Health Report, kiwango cha matumizi ya kondomu kimeshuka hadi chini ya kima cha asilimia tano.

Kulingana na data hiyo, licha ya umuhimu wake katika kuzuia magonjwa ya zinaa na mimba zisizotarajiwa, idadi kubwa ya watu wenye umri wa kati ya miaka 15 na 29 hupuuza matumizi ya kondomu wakati wa kujamiiana.

Mifano iliyotolewa katika ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika miaka ya hivi karibuni, matumizi ya kondomu yamepungua nchini Kenya katika miaka ya hivi karibuni, kiwango kikishuka kutoka asilimia nne mnamo 2021 hadi asilimia mbili pekee mnamo 2022.

Katika mwaka wa 2022 zaidi ya kandomu milioni 400 zilitumika nchini na makundi tofauti ya watu, tofauti na mwaka uliotangulia ambapo zaidi ya kondomu bilioni moja zilitumika.

Kati ya kondomu hizi milioni 400, milioni 112 zilitumika na watu wenye umri wa miaka 15 na 49, huku milioni 3.9 zikitumika na watu wenye umri kati ya miaka 50 na 64.

Vile vile, zaidi ya kondomu milioni 12 zilitumika na watu walioko katika ndoa kama njia ya kupanga uzazi.

Watu wanaoishi na Ukimwi, watu wenye nyeti za jinsia tofauti na watu wanaotumia dawa za kulevya walitumia zaidi ya kondomu milioni 265, zaidi ya milioni moja na zaidi ya kondomu milioni tano, mtawalia.

Kupungua huku kwa matumizi ya mipira ya kondomu kumeibua wasiwasi miongoni mwa wataalamu wa afya, kwa misingi kuwa ni muhimu katika uzuiaji wa maradhi ya zina na mimba zisizotarajiwa.

Kwa hivyo, wanasema ipo haja kwa kuimarishwa kwa uhamasisho kuhusu umuhimu wa watu wenye umri mdogo kutumia kinga wakati wa kufanya mapenzi.

Kulingana na viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) mwanamume mmoja anafaa kutumia kondomu 40 kwa mwaka.

Hata hivyo, nchini Kenya matumizi ya mipira hiyo miongoni mwa wanaume ni wastani wa 14 kwa mwaka.

Hii ina maana kuwa kampeni za uhamasisho kuhusu matumizi ya kinga katika kufanya mapenzi umeshuka, na hivyo watu wengi wanashiriki ngono bila kinga.

Baadhi ya wataalamu wanasema uhaba wa kondomu kutokana na utozaji wa ushuru kwa bidhaa hiyo, ni mojawapo ya sababu zinazochangia idadi ndogo ya watu kutumia mipira hiyo.

Hatua ya serikali kutoza ushuru kwa bidhaa hizo imechangia bidhaa hizo kuwa ghali kiasi kwamba wameshindwa kuimudu.

Wakenya walioozungumza na Taifa Dijitali walitoa sababu mbalimbali kuhusu sababu ya wao kuepuka kutumia kondomu.

Miongoni mwa sababu hizo ni bei ghali ya vifaa hivyo, unyanyapaa na dhana kwamba kondomu inashusha raha wakati wa kufanya mapenzi.