• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:25 PM
Ushuru wa Nyumba: Ruto apata ushindi wa kwanza bungeni

Ushuru wa Nyumba: Ruto apata ushindi wa kwanza bungeni

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto mnamo Jumanne alipata ushindi wa kwanza katika juhudi za serikali yake kuendelea kutoza Wakenya ushuru wa nyumba kufadhili mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu (AHP).

Hii ni baada ya Mswada wa Nyumba za Gharama Nafuu wa 2023 wa kuhalalisha ushuru huo, kupita katika hatua ya pili katika bunge la kitaifa mnamo Jumanne alasiri.

Katika kura ya moja kwa moja iliyopigwa baada ya kukamilika kwa mjadala kuhusu mswada huo, jumla ya wabunge 141 walipiga kura ya NDIO kuunga mkono mswada huo huku 58 wakipiga kura ya LA kuupinga.

“Ningependa kutangaza matokeo ya upigaji kura ambao umekamilika sasa hivi (jana Jumanne) kuhusu Mswada wa Nyumba za Gharama Nafuu wa 2023. Matokeo ni kama yafuatayo, upande wa Ndio ni wabunge 141 na wale waliopiga kura ya La ni 58. Jumla ya wabunge 199 walishiriki na hamna aliyesusia na hivyo upande wa ndio umeshinda,” Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula akatangaza.

Wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza walisherehekea ushindi huo kwa kuakisi agizo walilopewa na Rais Ruto katika mkutano wa Naivasha kwamba watumie idadi yao kuupitisha mswada huo tata.

Sasa mswada huo utashughulikiwa leo Jumatano alasiri katika hatua ya tatu ambapo wabunge watapata nafasi ya kuwasilisha marekebisho mbalimbali kwa mswada huo.

Marekebisho hayo yanajumuisha kuondolewa kwa hitaji ya kwamba wanunuaji wa nyumba hizo walipe amana (deposit) ya kima cha asilimia 10 ya thamani ya nyumba kabla ya kuruhusiwa kuzinunua.

Baada ya mswada huo kupitishwa katika Bunge la Kitaifa, utawasilishwa katika Seneti ambako utashughulikiwa ikizingatiwa suala la nyumba linahusu serikali za kaunti.

Mswada huo uliandaliwa na mrengo wa serikali baada ya Mahakama kuharamisha hatua ya serikali kuendelea kuwatoza Wakenya ushuru wa nyumba na kuitaja kama kinyume cha Katiba.

Katika uamuzi wa Novemba 26, 2023, majaji watatu wa Mahakama Kuu wakiongozwa na Daniel Majaji walisema ushuru huo unawabagua wafanyakazi wanaopokea mishahara kila mwezi kwa kutozwa asilimia 1.5 ya mishahara yao kila mwezi kufadhili mpango huo.

Majaji hao walipendekeza kuwa watu waliojiajiri pia washirikishwe katika ulipaji wa ushuru huo.

Mswada huo umepingwa na mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya ukisema ushuru huo wa nyumba unawaongezea Wakenya mzigo wa ushuru nyakati hizi ambapo makali ya kudorora kwa uchumi yanaawaumiza raia wengi wakiwemo wale wenye ajira.

  • Tags

You can share this post!

Kuchapa baada ya kuachana na Mulamwah kulifanya niende VCT...

Upekee wa kabati la Mswahili

T L