Usipotoa ushahidi, madai ya hongo yatabakia uvumi tu, viongozi wa Bunge wajibu Ruto
UONGOZI wa Bunge la Kitaifa umepuuza matamshi ya Rais William Ruto kuhusu madai ya hongo bungeni, ukisema ni tuhuma tu, na kumtaka atoe ushahidi wa madai hayo ya ufisadi.
Wakiongozwa na Spika Moses Wetang’ula, Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah, na Kiongozi wa Wachache Junet Mohammed, viongozi hao walisema yeyote anayewatuhumu wabunge kwa kupokea hongo lazima athibitishe madai hayo kabla ya hatua yoyote kuchukuliwa.
Akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Uongozi wa Bunge la Kitaifa uliofanyika Mombasa, Bw Wetang’ula alipuuza madai ya Rais Ruto kuhusu hongo bungeni na kwa wakati huo huo akatoa wito kwa wabunge kufanya kazi kurejesha imani ya wananchi kwa Bunge.
“Shaka imewekwa kuhusu uadilifu wetu kama Bunge. Sote tunafahamu mjadala wa hivi majuzi wa umma unaodokeza kuwa wabunge wamekuwa wakiitisha na kupokea pesa kama kishawishi ili kupitisha miswada ya sheria,” alisema Bw Wetang’ula.
Alisisitiza umuhimu wa uongozi wa uadilifu, akiwahimiza Wabunge kuongozwa na maadili yaliyoanishwa katika Ibara ya 73 ya Katiba.
“Masuala ya uadilifu si chaguo la kile kilicho rahisi bali ni chaguo la lililo sahihi. Kama viongozi, lazima tuongoze kama mfano kwa kudumisha uadilifu katika majukumu yetu tofauti,” alisema Spika Wetang’ula.
Aliongeza kuwa, “Tunaposhutumiwa kuhusu uadilifu, tujiulize ikiwa tunayatekeleza majukumu yetu kwa uwazi na bila upendeleo, na kuhakikisha maamuzi hayachochewi na ukabila, upendeleo au tamaa za ufisadi.
“Je, tunahudumu kwa kujitolea na kwa maslahi ya umma pekee? Haya ni maswali ya kibinafsi yaliyo msingi wa Katiba na ni lazima yawe mioyoni mwetu kila wakati.”
Kwa upande wake, Bw Junet alisema kila mtu ana haki ya kutoa maoni, lakini changamoto ni kuthibitisha anachosema.
“Madai ya hongo yanapaswa kuthibitishwa. Tunatoa changamoto kwa wale wanaounga mkono madai hayo kuwasilisha ushahidi bungeni ili uongozi uchukue hatua,” alisema Bw Junet.
Katika mkutano huo wa siku tatu, viongozi wa Bunge wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yanayokumba Bunge.
Wakati wa ufunguzi rasmi wa mkutano huo, Bw Wetang’ula alitetea Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (NG-CDF), akisema hazina hiyo si ya serikali za kaunti na magavana hawastahili kuithibiti kwani si sehemu ya mapato ya kugawiwakaunti bali ni sehemu ya fedha za Serikali Kuu.
“Lazima tulinde mafanikio ya NG-CDF. Napongeza wabunge kwa kuongoza kupitisha Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya Kenya wa 2025 unaolenga kuingiza NG-CDF kwenye Katiba,” alisema Bw Wetang’ula.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Bw Ichung’wah na Mbunge wa Suba Kaskazini, Bi Millie Odhiambo, walioweka wazi kuwa watailinda hazina hiyo.
“Nafahamu kiongozi wa chama changu Bw Raila Odinga anataka fedha hizo ziwe sehemu ya ugatuzi, lakini huo ni msimamo na maoni yake binafsi. NG-CDF ni suala la kitaifa na Katiba imeweka wazi kuwa si ya kaunti na magavana hawastahili kuzipokea kwani si sehemu ya mapato ya mgao wa kaunti,” alisema Bi Odhiambo.
Wakati wa mkutano huo, hoja pia zilitolewa kuhusu taratibu za shughuli za Bunge na changamoto ya kutokuwepo kwa idadi ya kutosha ya wabunge, hali ambayo imechelewesha kupitishwa kwa miswada mingi.
Bw Wetang’ula alieleza hofu yake kuwa ukosefu wa idadi ya kutosha ya wabunge bungeni katika miezi saba iliyopita umesababisha kucheleweshwa kwa mijadala ya miswada iliyosubiriwa kwa muda mrefu.
“Ninatambua kuwa mnalo jukumu katika maeneo yenu ya uwakilishi, lakini pia mnapaswa kuhakikisha hamtelekezi majukumu yenu bungeni. Wenyeviti wa Kamati lazima wapatie kipaumbele kazi ya kutunga sheria na kuisimamia Serikali ndani na nje ya Bunge. Tumekuwa na changamoto ya idadi ndogo ya wabunge hata wakati wa shughuli muhimu za Bunge, na mara nyingine wenyeviti wa kamati husika hushindwa kusukuma masuala yao bungeni,” alisema Spika.
Aliongeza kuwa hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi miezi ijayo huku wabunge wakilenga kampeni katika maeneo yao kuelekea uchaguzi mkuu.
“Tunatarajia ratiba nzito kwa wabunge katika maeneo yao, wengine wakitafuta kuchaguliwa tena na wengine wakilenga nyadhifa nyingine. Lakini nawasihi wabunge kuweka mizani ya haki kati ya kazi za maeneo yao na majukumu ya Bunge na kamati zake, ili kuepuka ucheleweshaji usio wa lazima wa shughuli za Bunge. Ili Bunge litimize wajibu wake, uwepo wa wabunge ni wa lazima,” alisema.
Viongozi hao pia walieleza masikitiko yao kuhusu ushiriki mdogo wa wabunge katika ripoti mbalimbali, huku baadhi yao hata wakiwa hawajui yaliyomo katika ripoti hizo.
Wanatarajiwa kujadili ripoti hizo na kuweka mikakati madhubuti ya kushughulikia mzigo wa kazi ulio Bungeni.