Habari za Kitaifa

Utalii: Kenya yavuna joto la siasa likiwaka kwa majirani Uganda na Tanzania

Na WINNIE ATIENO December 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ENEO la Pwani linashuhudia ongezeko kubwa la watalii, kipindi cha likizo za Krismasi na Mwaka Mpya kikiwa kinaanza.

Wadau wa sekta hiyo wanahusisha ongezeko hilo na miundomsingi bora ya usafiri nchini, mikakati maalumu za utangazaji, pamoja na joto la kisiasa katika nchi jirani kama Uganda na Tanzania, ambalo huenda limewafanya watalii kuelekeza safari zao Kenya.

Nafasi zimejaa katika hoteli nyingi hadi baada ya Mwaka Mpya, huku maeneo maarufu ya kitalii kama vile Diani, Malindi na Mombasa yakiendelea kufurika wageni.

Watoa huduma za usafiri ikiwemo kampuni za mabasi, mashirika ya ndege na Reli ya SGR pia wanavuna kutokana na ongezeko la abiria huku SGR ikiongeza safari za kukidhi mahitaji yaliyoongezeka.

“Tumeona ongezeko kubwa la watalii wanaofurika Pwani ya Kenya na hoteli nyingi zimejaa. Hii imetokana na joto la kisiasa katika nchi jirani za Tanzania na Uganda. Pia tuko katika msimu mkuu ambao utaendelea hadi mapema mwaka ujao,” alisema mwenyekiti wa Baraza la Utalii Mombasa, Dkt Sam Ikwaye.

Meneja Mkuu wa Hoteli ya Travellers Hilary Siele, alithibitisha kuwa, ongezeko hilo la watalii limefanya hoteli nyingi kujaa.

Wadau pia waliihusisha hali hiyo na sera ya anga wazi iliyoanzishwa na serikali ya kitaifa, ambayo imewezesha mashirika mengi ya ndege kutua moja kwa moja katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi (MIA).

Viongozi wa Pwani wamekuwa wakisukuma kwa muda mrefu sera hiyo ili kuruhusu ndege za kimataifa kutua moja kwa moja Mombasa na kufufua sekta inayodorora.

Miongoni mwa mashirika mapya yanayonufaika na sera hiyo ni RwandAir, iliyorejea karibuni, na Freedom Airlines, iliyoanzisha safari tatu kwa wiki.

“Mashirika mapya ya ndege yataboresha usafiri hadi kwa jiji letu na kuongeza fursa za kiuchumi,” Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli na Wahudumu Kenya (KAHC) Mike Macharia, alisema huduma za Kenya ni za kiwango cha juu na ndizo zinazovutia wageni wengi.

Alitaja ustadi wa wataalamu wa Kenya wanaofanya kazi kwenye meli za kitalii, hoteli, mashirika ya ndege na viwanja vya ndege duniani.

Meneja Mkuu wa Diamonds Leisure Beach and Golf Resort, Bw Andrew Cook, alisema hoteli yake imejaa, na imevutia wageni wa ndani na nje hasa kutoka Ulaya.

Alihusisha ongezeko la watalii na miundomsingi bora ya barabara na anga, ikiwemo barabara ya Dongo Kundu.

Meneja Mkuu wa Hoteli ya Sapphire, Bw John Yegon, alisema hoteli yake inanufaika na huduma ya reli inayosafirisha abiria kutoka kituo cha SGR cha Miritini hadi katikati ya jiji la Mombasa.

Wakati uo huo, vyombo vya usalama vimeimarisha doria na ulinzi kuhakikisha usalama wa wenyeji na wageni msimu huu wa sikukuu.

Kamanda wa Polisi Ukanda wa Pwani, Bw Ali Nuno, aliwaondolea hofu wananchi.

“Tumeimarisha usalama katika pwani ya Kenya. Tunawahakikishia watu kuwa wanaweza kusherehekea msimu wa sikukuu bila matukio. Ni salama kabisa,” alisema.

Sekta ya utalii pia imenufaika pakubwa kutokana na shughuli za hadhi ya juu kama vile Mashindano ya ‘2025 East Africa Safari Classic Rally’.

Mashindano hayo yalivutia washiriki 59, ambapo 48 walikuwa wametoka zaidi ya nchi 75. Madereva kutoka Rwanda, Tanzania, Zambia na Angola walishiriki.

Mwenyekiti wa mashindano hayo, Bw Joey Ghose, alisema mashindano hayo, ambayo gharama yake ni Sh517 milioni na pia yalivutia madereva maarufu wa mbio za magari ulimwenguni na washiriki vijana waliowekeza zaidi ya Sh129 milioni kila mmoja kushiriki.