Habari za Kitaifa

Utashuka tu, Raila amwambia Ruto kuhusu ushuru

January 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA SHABAN MAKOKHA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga amesisitiza kuwa Rais William Ruto hana budi ila kupunguza mateso ya Wakenya mwaka huu badala ya kulaumu upinzani kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake za uchaguzi.

Bw Odinga alisema anatarajia mwaka huu wa 2024 utakuwa bora kwa raia “kuliko 2023 ambao serikali ya Kenya Kwanza ilifanya maisha ya wengi kuwa magumu”.

Alikosoa serikali kwa kupuuza vilio vya wananchi waliopiga kura kwa kuvutiwa na ahadi zake Rais Ruto.

Akizungumza akiwa Kakamega jana, kiongozi huyo wa ODM alisema Dkt Ruto amesahau vijana, mama mboga, bodaboda na wahudumu wa juakali ambao anabebesha mzigo wa gharama ya maisha ilhali aliahidi kuwapa umuhimu.

“William Ruto aliahidi Wakenya wote kuwa wangekuwa sehemu ya serikali yake. Leo wanatazama serikali kwa Viusasa. Hazungumzi tena juu yao. 2024 unapaswa kuwa mwaka wa mabadiliko, mwaka wa gharama nafuu ya maisha, kufanya maisha kuwa nafuu na kuwarejeshea Wakenya tabasamu,” akasema Bw Odinga.

Alimshauri Rais Ruto kutambua mahitaji ambayo mwananchi wa kawaida anataka yapewe umuhimu na kupunguza ushuru akidai Wakenya wengi wanateseka na kufadhaika kwa sababu hawana chakula, malazi na hawawezi kumudu huduma bora za afya.

“Mwaka unapoanza, kwanza tuzingatie masaibu ya Wakenya ambao hawana uwezo wa kutia tonge mdomoni kabla ya kufikiria mambo mengine ili 2024 uwe bora kuliko 2023,” akaongeza.

Haya yanajiri baada ya kiongozi huyo wa Azimio awali kutoa orodha ya hatua ambazo mrengo wake utachukua dhidi ya serikali
ambazo ni pamoja na kuongoza maandamano iwapo serikali itashindwa kupunguza gharama ya maisha.

“Ninatoa wito kwa Wakenya kujiandaa kwa nyakati ngumu huku kukiwa na uwezekano wa kuandamana kushinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha,” akasisitiza.

Baadhi ya wafuasi wake waliojaza uwanja wa michezo wa Bukhungu walimtaka aitishe maandamano mara moja.

“Tunataka maandano!! Tutangazie maandamano!!! Tunataka maandamano, tuitishie maandamano,” walisema.