Utata wazuka kuhusu pesa zilizokusanywa barabara ya Nairobi Express Way
WABUNGE sasa wanataka serikali kuweka wazi pesa zilizokusanywa kutoka barabara kuu ya Nairobi Expressway, huku kukiwa na taarifa zinazokinzana kuhusu fedha ambazo zimekuwa zikikusanywa almaarufu ‘toll fees’.
Tangu kuzinduliwa kwake na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta mnamo Julai 2022, hakuna taarifa ya wazi iliyotolewa kuhusu ukusanyaji na matumizi ya pesa ya barabara hiyo iliyogharimu Sh88 bilioni kujenga.
Seneta wa Kisii Richard Onyonka alidokeza kuwa ripoti za hivi majuzi za kifedha zilionyesha mienendo ya kutiwa wasiwasi ambayo inahitaji kuchunguzwa.
Alisema kumekuwa na habari zinazokinzana kuhusu jinsi barabara hiyo imekuwa ikitumiwa, huku akitoa wito kwa kamati ya Seneti kuhusu Barabara na Uchukuzi kuanzisha uchunguzi kuhusu utendakazi wa kifedha wa mradi huo.
Kwa hivyo, kamati inayoongozwa na Seneta wa Kiambu Karungo Thang’wa imetwikwa jukumu la kudadisi na kutoa ripoti kuhusu fedha zilizokusanywa katika barabara hiyo tangu kuzinduliwa kwake.
Hii itahusisha kulinganishwa kwa makadirio dhidi ya kiwango halisi kilichokusanywa.
Kamati pia inatarajiwa kueleza mikakati ya kukabiliana na upungufu wa utendaji kazi, kuongeza mapato ya ushuru, na usimamizi wa gharama za ulipaji wa mkopo kwa ufanisi.
“Ripoti za hivi majuzi za kifedha zinadokeza kuwa kuna haja uchunguzi ufanywe kuhusu matumizi ya pesa zinazokusanywa kutoka barabara hiyo,” akasema Bw Onyonka.
Ripoti iliyowasilishwa Bungeni Novemba mwaka huu ilionyesha kuwa barabara hiyo ilipata hasara ya Sh1.2 bilioni katika kipindi cha kati ya Julai 2023 na Juni 30, 2024.
Takwimu kutoka kwa Hazina ya Kitaifa zilifichua kuwa mradi huo ulipata Sh4.6 bilioni wakati ambapo gharama ya shughuli za mwekezaji huyo kutoka China ilikuwa Sh5.8 bilioni.
Hata hivyo, alipokuwa akizungumza Februari 2023, afisa mkuu mtendaji wa Moja Expressway Steve Zhao alisema barabara hiyo imekusanya takriban Sh2 bilioni za ada za ushuru tangu kuzinduliwa Julai 2022.
Alisema kwa wastani watu hutumia Sh200 kutoka sehemu moja ya kutokea hadi nyingine lakini baadhi ya taarifa zimesema madereva hulipa hadi Sh417 kutumia barabara hiyo.
Kufikia Februari 7, 2023, magari milioni 10 yalikuwa yametumia barabara hiyo na wastani wa magari 50,000 yakiitumia mara mbili kila siku.
Lakini pia kumekuwa na ripoti zinazokinzana kuhusu idadi kamili ya magari yanayotumia barabara hiyo huku baadhi ya ripoti zikiweka idadi hiyo kuwa wastani wa magari 11,000 kila siku.
Barabara ya Nairobi Expressway ni mradi muhimu wa miundombinu ulioanzishwa 2022 chini ya muundo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Barabara hiyo inaendeshwa na Kampuni ya China Road and Bridge Corporation (CRBC) chini ya makubaliano ya miaka 27 ili kurejesha uwekezaji wake na inatarajiwa kupata faida inayokadiriwa ya Sh106.8 bilioni kwa miaka 27 itakayomiliki barabara hiyo.