Utekaji wavuka boda: Jinsi Serikali za EAC zimeungana kunyamazisha wakosoaji
UTEKAJI nyara sasa unaonekana kama mojawapo ya silaha zinazotumika na serikali za Afrika Mashaki kujaribu kuwatia woga na kuwanyamazisha wakosoaji wao.
Mwanaharakati Mkenya, Mwabili Mwagodi ndiye wa hivi punde zaidi kupatwa na ukatili huo mnamo Jumatano wiki jana aliporipotiwa kutekwa nyara jijini Dar es Salam, Tanzania.
Bw Mwagodi, maarufu kama TL Elder, kwenye mtandao wa X, amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais William Ruto kupitia jukwaa hilo ambako anafuatwa na zaidi ya watu 76,000.
Mwanaharakati huyo ambaye amekuwa akifanya kazi katika mkahawa wa Amani Beach Hotel, eneo la Kigamboni, Tanzania, aliachiliwa jana baada ya kuzuiliwa kwa siku nne.
Aliachiliwa katika eneo la Lunga Lunga, baada kuteswa huku akihojiwa kuhusu masuala ya kisiasa na maandamano ya Gen-Z ya Juni 2024.
Bw Mwagodi aliwahi, mwaka huo, kuongoza maandamano nje ya kanisa moja ambako Rais Ruto alihudhuria ibada mjini Nyahururu, Laikipia mwaka jana.
Baada ya hapo familia yake ilitembelewa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na kuwaambia wazazi wake wamshauri kukoma kuikosoa serikali.
“Mnamo Oktoba 2024, wazazi wetu walitembelewa na wageni waliojitambulisha kama maafisa wa DCI na wakawaonya kwamba Mwagodi ajiepushe na maandamano ya Gen-Z na ukosoaji wa serikali,” akasema Isabella Kituri, dadake Mwagodi.
Kutekwa nyara kwa mwanaharakati huyo kunajiri miezi miwili baada ya masaibu sawa na hayo kumpata mwanaharakati Boniface Mwangi na mwenzake, raia wa Uganda, Bi Agather Atuhaire.
Wawili hao walikamatwa, kuzuiliwa na kuteswa jijini Dar es Salam, mnamo Mei.
Walifika nchini humo kuhudhuria kikao cha kusikilizwa kwa kesi dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu.
Mnamo Januari 12, 2015, Maria Sarungi, Mtanzania na mwanahabari, aliyetoroka nchi yake baada ya kutishwa, alitekwa nyara katika mtaa wa Kilimani, Nairobi.
Aliachiliwa huru saa chache baadaye kutokana na presha kutoka kwa wanaharakati wa kutetea haki za binadamu.
Mnamo Novemba 17, 2024, kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Dkt Kizza Besigye alikamatwa jijini Nairobi na kusafirishwa hadi nchini mwake Uganda kushtakiwa kwa uhaini.
Ongezeko la visa hivi katika ukanda wa Afrika Mashariki limevutia shutuma kutoka kwa Chama cha Mawakili kutoka nchi za Jumuiya ya Madola (CLA).
Chama hicho kinataka serikali za Kenya, Uganda na Tanzania, kutumia mbinu mbadala za kupambana na wakosoaji; mbinu zisizokiuka haki za kimsingi za wahusika.
“CLA imeelezea hofu kuhusu mtindo wa utekaji nyara na mateso ya wanaharakati na wakosoaji wa serikali, hasa katika nchi za Kenya, Uganda, and Tanzania,” CLA akasema kwenye taarifa.
Chama hicho kilieleza kuwa mbali na wanaharakati na viongozi wa upinzani, wengine wanaolengwa ni vijana wanaoshiriki maandamano na hata wanahabari.
Kulingana na CLA, ambacho ni chama kilichoundwa kuendeleza utawala wa sheria katika mataifa wanachama wa Jumuiya ya Madola, ilieleza kuwa nchi hizo tatu zinatumia mbinu hiyo ya utekaji nyara kupunguza ukosoaji na kuwatia woga watu wanaotekeleza haki yao ya kufanya maandamano na kuhakikisha kuwa serikali zinawajibika.
CLA inasema mtindo wa kumzuilia mtu kinyume cha sheria, alivyofanyiwa Mwagodi, ni kielelezo cha ukiukaji wa haki za kimsingi za walengwa.
Kipengele cha tano cha Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Watu kinasema kuwa kila watu waliokamatwa hawapaswi kunyimwa haki zao za kimsingi, kama vile kufikiwa na mawakili wao.
Mkataba huo unapiga marufuku dhuluma zozote dhidi ya binadamu, utumwa, mateso na adhabu ya kikatili.