Habari za Kitaifa

Uzembe wa walimu kuwasilisha data yenye dosari wafanya maelfu kukosa ufadhili

Na MERCY SIMIYU September 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MAELFU ya shule za upili nchini bado hazijapokea ufadhili wa serikali baada ya kubainika walimu wakuu waliwasilisha data yenye dosari kwa Wizara ya Elimu.

Wizara imekuwa ikiendelea kuhakiki data na inawasilisha pesa tu kwa shule ambazo zimeidhinishwa.

Data ambayo Taifa Leo imepokea inaonyesha kuwa shule 719 ziliwasilisha maelezo yasiyo sahihi ya benki na kuzua hofu kuwa hela zitachelewa zaidi au kuelekezwa akaunti isiyofaa.

Shule 900 nazo ziliwasilisha data au maelezo ya wanafunzi yakiwa hayajakamilika.

Baadhi ya shule nazo ziliwasilisha stakabadhi kwenye muundo usiofaa na huku nyingine zikiambatanisha fomu wazi za benki na nambari zisizowiana za wanafunzi.

Kuchelewa kwa ufadhili huo kunatokea wiki nne baada ya muhula wa tatu kuanza.

Shule za msingi, sekondari na sekondari za chini zote zimeathirika huku walimu wakuu wakionya kuwa ukosefu wa fedha tayari unaathiri shughuli za kila siku.

“Hatuwezi kuwalipa wawasilishaji bidhaa kwa wakati na kushiriki shughuli ambazo si za masomo. Hali inaendelea kuwa mbaya,” akasema mkuu mmoja wa shule.

Kaunti ambazo zimeathirika zaidi ni Bungoma, Kisii, Busia, Baringo, Kericho, Kakamega, Kitui na Nairobi.

Kaunti nyingine ni Bomet, , Elgeyo Marakwet, Embu, Garissa, Homa Bay, Isiolo, Kajiado, Kiambu, Kilifi, Kirinyaga, Kisumu, Kwale, Laikipia, Lamu, Machakos, Makueni, Mandera, Marsabit, Meru, Migori, Mombasa, Murang’a,, Nakuru, Nandi, Narok, Nyamira, Nyandarua, Nyeri, Samburu, Siaya, Taita Taveta, Tana River, Tharaka Nithi, Trans Nzoia, Turkana, Uasin Gishu, Vihiga, Wajir na Pokot Magharibi.

Kutolewa kwa mgao wa muhula huu na zaidi kunahusishwa na kuhakikiwa na kuthibitishwa kwa maelezo ya shule.

Maelezo hayo yanalenga usimamizi, idadi ya waliojisajili, maelezo ya akaunti za benki na shughuli nyingine ambazo zimekuwa zikiendelea tangu kuanza kwa muhula huu.

Alipofika mbele ya Kamati ya Elimu Bungeni, Katibu katika Wizara ya Elimu Julius Bitok alisema wamegundua kulikuwa na zaidi ya wanafunzi hewa 50,000 katika shule za sekondari.

Hali imezua maswali kuhusu usajili na uwazi katika asasi ambazo zinafadhiliwa na serikali.

Profesa Bitok alisema ufichuzi huo uligunduliwa wakati wa shughuli za kuhakiki data za shule ambazo zinaendelea na zimefikia katikati.

“Hadi sasa, tumesambaza hela kwa shule 17,500 ambapo 5,500 ni za sekondari kati ya 9,500, shule 5525 ni za sekondari ya chini na shule spesheli 600,” akasema Profesa Bitok.

“Tumebaini kuwa, kuna zaidi ya wanafunzi hewa 50,000 wa sekondari. Ukweli ni kuwa, takwimu hizo haziingiliani na ni wazi idadi ya wanafunzi ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa,” akasema.

Ukora ambao umefichuliwa imebainika husababisha hasara ya Sh1.1 bilioni kila mwaka na ni Sh4.4 bilioni ambazo serikali imelaghaiwa kwa muda wa miaka minne iliyopita.

Alisema data ya shule za msingi na zile za sekondari za chini bado zinajumuishwa huku ikibainika ukora wa wanafunzi na shule hewa umepatikana umekolea sana kwenye shule za sekondari.

Profesa Bitok alifichua kuwa, asilimia 60 ya shule 32,000 kote nchini zimeidhinishwa, zikatumiwa pesa huku uhakiki wa shule zilizosalia ukiwa bado unaendelea.

“Tunatarajia kuwa shule 20,000 zitakuwa zimekamilishiwa mchakato wote na wiki jana shule 15,000 zilikuwa zimeshughulikiwa. Hadi sasa, tumetuma zaidi ya asilimia 60 ya mgao wa Sh23 bilioni ambazo ni Sh13 bilioni na mchakato huo bado unaendelea,” akasema.

Alifichua kuwa ni wikendi tu ambapo mchakato huo ulikuwa chini baada ya intaneti kuvurugika kutokana na kukatika kwa nyaya za intaneti; tukio lililositisha shughuli za idara mbalimbali za serikali.

Haya yanatokea huku Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu Bungeni Julius Melly akiwataka wabunge na maafisa wa elimu wachukue hatua kali dhidi ya wale ambao wanahusika katika kubuni shule feki na kupora raslimali za serikali.

Bw Melly alisema sakata hiyo haipaki tope tu serikali bali pia imesababisha serikali kupoteza mabilioni ya fedha.

“Hatuwezi kuruhusu pesa za umma zifyonze kupitia shule hewa kubuniwa. Kila anayepatikana na hatia lazima achukuliwe hatua kali kwa sababu watoto wetu wanahitaji kushughulikiwa vyema, kila shilingi ambayo imetengewa sekta ya elimu lazima inufaishe mwanafunzi,” akasema Bw Melly.

Alipokutana na walimu Jumamosi iliyopita Ikulu ya Nairobi, Rais William Ruto aliamrisha Wizara ya Elimu na ile ya Fedha zielewane kuhusu jinsi ya kutoa mgao ili ioane na kalenda ya masomo.