Habari za Kitaifa

Vijana wanavyounda hela kwa kupiga seti kwenye matatu

January 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MAOSI

VIJANA wengi Jijinia Nairobi wanatengeneza hela kwa kupiga seti kwenye matatu za Uchukuzi wa Umma (PSV).

Kwa sababu hakuna sheria ya kuwadhibiti, ni zoezi ambalo limeshika kasi katika steji maarufu za Tea Room, Railways, Afya Centre na Machakos Country Bus.

Hata hivyo ni jambo ambalo limekuwa likipokelewa vibaya na wasafiri wakitaka serikali iwachukulie hatua kali wahusika kwa kuwapotezea muda.

Alice Wangare ambaye hutumia matatu kati ya Kamukunji na Nairobi anakiri kwamba siku hizi, kwa sababu ya kupiga seti, wizi umeongezeka ndani ya matatu.

Kulingana na Alice, baadhi ya watu wamekuwa wakijifanya ni abiria lakini lengo kuu ni kuiba simu na mizigo.

Isitoshe anawalaumu makanga kwa kushirikiana na vijana wa kupiga seti, ikizingatiwa kuwa baadhi yao ni vijana wanaorandaranda mitaani.

“Labda wamekuwa wakiwasaidia madereva na makanga kujaza gari, kwa sababu biashara ya matatu jijini Nairobi, Nakuru na Baringo zinakumbana na ushindani mkali,” anasema.

Wakati mmoja anakumbuka aliwahi kuabiri basi kuelekea Machakos, kwenye kituo cha Machakos Country Bus ila ilimchukua saa tano kabla ya basi kuondoka.

Bw Reuben Some kutoka kituo cha Railways ambaye amekuwa akifanya kazi ya kupiga seti anasema Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya zimeisha kwa hivyo kazi sio nzuri.

Anasema hii ni kazi kama nyinginezo muradi mkono unaenda kinywani.

Kwa siku Some ambaye ni mzaliwa wa Tinderet Kaunti ya Nandi anaweza kutengeneza kati ya Sh400-600 ambazo humsaidia kulipa kodi na kununua chakula.

Some anasema biashara yenyewe sio haramu kwa sababu anatumia akili kuwasaidia wamiliki wa matatu kujaza magari yao kwa malipo maalum.

Anasema ni jambo ambalo hufanyika katika takriban kila steji ya mabasi nchini na hakuna sheria ambayo imewekwa kuzuia seti.

Aidha, ni jambo ambalo limeacha vyombo vya usalama kujikuna kichwa kutokana na kushuhudiwa kwa idadi kubwa ya vijana wanaojihusisha na uhalifu kwenye stesheni za mabasi.