Vijana wawili wateketezwa kwa madai ya kupora nyumba za waliosafiri mashambani
VIJANA wawili wanaoshukiwa kuwa wezi walichomwa hadi kufa na umma katika Mtaa wa Kabiria, Wadi ya Riruta, Eneo bunge la Dagoretti Kusini asubuhi ya Alhamisi, huku mmoja akinusurika baada ya kutoroka.
Inaaminika kuwa watatu hao walikuwa wakivunja nyumba za watu waliosafiri mashambani na kuiba mitungi ya gesi na bidhaa nyingine muhimu.
Wawili hao, ambao majina yao hayakutambulika mara moja, walikamatwa na majirani wakijaribu kuvunja nyumba nyingine huku wakiwa na mitungi miwili ya gesi.
Kulingana na walioshuhudia tukio hilo, watatu hao walionekana wakifika katika ploti hiyo majira ya saa kumi na mbili asubuhi.
Mary Wanjiku, ambaye ni jirani, aliona watatu hao wakivunja nyumba moja ya mpangaji. Aliwaarifu majirani wenza ambao walipiga kelele.
“Tumekuwa tukishuhudia wizi mwingi, hasa wakati wa sherehe za Krismasi,” alisema Wanjiku.
“Tulipoona wanavunja, tuliita msaada, na watu walikimbia haraka.”
Wakazi wa eneo hilo walisema wamechoshwa na visa vya wizi vya mara kwa mara. Walifuata wezi hao na kukamata wawili walipokuwa wakijaribu kutoroka.
Licha ya maombi yao ya kutaka kuonewa huruma, umati uliwapiga na hatimaye kuchoma wawili hao kwa kutumia petroli na magurudumu.
Bw James Kamau, ambaye nyumba yake iliibiwa siku mbili zilizopita, alielezea kukata tamaa na kulamu maafisa kukosa kushughulikia uhalifu huo.
“Walichukua mitungi yangu ya gesi na baadhi ya vitu vya nyumbani. Najihisi kukosa msaada kwa sababu hii siyo mara ya kwanza. Tunaripoti kwa polisi, lakini hakuna anayeonekana kujali,” alisema.
Bi Margaret Atieno, alikumbuka jinsi wezi walivyovamia nyumba yake wiki iliyopita.
“Tulikwenda shambani kwa Krismasi, tukarudi na kupata mlango umevunjwa na nyumba ikiwa tupu. Hatujihisi salama tena,” alilalamika.
Polisi walifika katika eneo la tukio dakika chache baada ya tukio hilo, wakitawanya umati na kuokoa miili ya washukiwa iliyosalia.
Afisa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Riruta, Sarah Kimsar, alikemea vikali vitendo vya sheria mikononi mwa umma na kuhimiza wakazi kuripoti visa hivyo badala ya kuchukua sheria mikononi mwao.
“Tunafahamu machungu yanayotokana na ongezeko la visa vya wizi, lakini adhabu ya umati siyo suluhisho,” alisema Kimsar.
“Tunaendelea kuchunguza tukio hili na tunawafuata washirika wa huyo aliyekimbia,” aliongeza Kimsar.
Aliongeza kuwa katika msimu huu wa sherehe, visa vya wizi vilivyotokea katika eneo hilo vitashughulikiwa haraka na maafisa wa polisi ambao wanajitahidi kuwakamata wahusika.
Hata hivyo, viongozi wa eneo hilo walihimiza wakazi na wamiliki wa nyumba kuchukua hatua za kuzuia wizi, kama vile kuajiri walinzi au kutoa taarifa kwa majirani wanaposafiri kwa kipindi cha sherehe.
Miili ya wawili hao ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya City Mortuary, Nairobi.