Viongozi ODM wataka Sifuna sasa atimuliwe
BAADHI ya viongozi waliochaguliwa kupitia chama cha ODM sasa wanamtaka Seneta Edwin Sifuna aondoke iwapo hataki Serikali Jumuishi.
Jumanne usiku, Bw Sifuna kwenye mahojiano na runinga moja nchini, alishambulia Serikali Jumuishi na kusema upinzani hautaunga azma ya muhula wa pili ya Rais William Ruto.
Hata hivyo, viongozi hao kutoka Kaunti ya Nairobi wakiongozwa na Mbunge wa Makadara, Bw George Aladwa, wamesema wamemchoka Bw Sifuna na wakati umefika ambapo anastahili kuondoka katika chama hicho.
Bw Aladwa ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi, alisema kuwa Bw Sifuna anaendeleza dhana kuwa matamshi yake yameidhinishwa na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ilhali si uhalisia wa mambo.
“Kwenye mahojiano hayo, alikuwa anayatoa matamshi hayo kama mtu binafsi wala si kiongozi wa chama. Sisi tunafuata mwelekeo wa Rais Ruto na Bw Odinga na kama Sifuna hataki mwelekeo huo basi yupo radhi kuondoka ODM,” akasema Bw Aladwa.
Hata hivyo, alisema jinsi Bw Sifuna amekuwa akiongea inaonyesha wazi kuwa ODM ni chama kinachovumilia maoni kinzani japo akasikitika kuwa mwelekeo ambao ameuchukua seneta huyo sasa hauvumiliki tena.
“Sisi tunafuata makubaliano kati ya Rais na Raila ambayo Sifuna mwenyewe aliyatia saini. Iwapo anaona kuwa sasa hayana maana basi ajiondoe chamani na kusaka kingine ambako ataendeleza siasa zake za kushambulia serikali,” akaongeza Bw Aladwa.
Akiongea wakati wa mahojiano hayo, Bw Sifuna alisema ODM haihusiki kivyovyote katika mpango wa kuhakikisha Rais Ruto anachaguliwa kwa mara ya pili mnamo 2027.
Alienda hatua moja zaidi na kuapa kuwa atamuunga mkono mwaniaji mwengine ambaye atahakikisha Rais Ruto anahudumu kwa muhula mmoja pekee.
Bw Aladwa akiwa ameandamana na viongozi wa ODM Nairobi, alisema chama hicho kishaweka wazi kuwa kitaunga kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto.
“Sisi hatutapoteza dira na hata Sifuna aseme nini, hatutatetereka. Kile ambacho anakisema katika mahojiano hata kwenye mikutano hakina mashiko. Sifuna hazungumzi kwa niaba ya chama,” akaongeza.
Kando na Bw Aladwa, Gavana wa Homa Bay, Bi Gladys Wanga na Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi, wakiongea Homa Bay wikendi, walisema kuwa wapo nyuma ya Rais hadi 2032.
Wawili hao walisema wanasiasa wanaompiga vita Rais Ruto ni wale ambao hawafurahii maendeleo ambayo yamekuwa yakishuhudiwa Nyanza.
Duru kutoka ODM zinaarifu kuwa baadhi ya wanasiasa wandani wa Bw Odinga, wanamshinikiza amfute Bw Sifuna kutoka kwa wadhifa wake.
“Sifuna lazima aanze kuyachunga matamshi yake kwa sababu baadhi yetu tumeanza kuhisi anatumika na upinzani kusambaratisha udhabiti wa chama chetu,” akasema mmoja wa wabunge wa ODM ambaye hakutaka kutajwa.