Habari za Kitaifa

Viongozi wa kidini wahimiza amani, uongozi unaojali raia Pasaka ikianza

Na  WAANDISHI WETU April 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAELFU ya waumini wa Kanisa Katoliki kutoka maeneo mbalimbali nchini Kenya waliungana na Wakristo wengine duniani kuadhimisha Ijumaa Kuu, huku viongozi wakikemea ufisadi, kupanda kwa gharama ya maisha na kuhimiza amani na uwiano.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Mombasa, Martin Kivuva, amewalaumu viongozi wa kisiasa kwa kile alichokitaja kuwa ubadhirifu wa mali ya umma na uongozi usiojali wananchi, akisema hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuyumbisha uchumi na kuongeza mateso kwa wananchi wa kawaida.

Akizungumza wakati wa ibada ya Ijumaa Kuu Jijini Mombasa, Askofu Kivuva, alisema kuwa Wakenya wengi wanahangaika kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu, huku viongozi wakizidi kujinufaisha kwa njia zisizo halali.

“Viongozi wanapaswa kuepuka mienendo inayoturudisha nyuma. Matumizi mabaya ya mali ya umma ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchi,” alisema kwa masikitiko, akisisitiza haja ya viongozi kuwajibika kwa wananchi wanaowahudumia.

Askofu huyo alisema gharama ya maisha imepanda kwa kiwango kisichovumilika, hali inayowafanya raia wengi kushindwa kumudu mahitaji ya kila siku.

“Uchumi wa taifa hauvutii. Bei ya bidhaa muhimu imepanda kwa kiwango kikubwa,” aliongeza.Katika hotuba hiyo, Askofu Kivuva pia alizungumzia suala la mshikamano wa kitaifa, akiwasihi Wakenya kudumisha amani na kuepuka migawanyiko ya kisiasa na kidini. Alisema taifa linahitaji maombi, mshikamano, na uongozi wa kutanguliza ustawi wa raia.

“Ingawa Kenya ina dini mbalimbali, hatupaswi kugawanyika. Sisi ni jamii moja na wote tunamwamini Mungu. Tujiepushe na kubaguana,” alisema.Aliwataka vijana kutokubali kutumiwa kuzua vurugu, akiwakumbusha kuwa wao ndio mustakabali wa taifa.

“Tunaombea nchi yenye upendo. Vijana waepuke kutumiwa kuharibu taifa. Tujitahidi kudumisha amani na utulivu,” alisema.Katika ujumbe wake wa Pasaka, Rais William Ruto pia aliwahimiza Wakenya kudumisha umoja, amani na mshikamano wa kitaifa, akisema msimu huu wa kiroho ni fursa ya kutafakari upendo wa Kristo na kuchukua hatua za kujenga taifa lenye utu.

Katika jiji la Kisumu, Padri Fredrick Odhiambo alihimiza Wakenya kudumisha amani, upendo na msamaha, akisisitiza umuhimu wa familia kujenga umoja wa kweli.


 “Familia zipatane. Tuishi kwa amani. Tusijenge wivu. Tusimame dhidi ya giza na mgawanyiko,” alisema Padri Odhiambo.Katika Kaunti ya Siaya, Apostle Elijah Onyango wa Jesus Shalom Ministries aliwataka wananchi kumrudia Mungu kwa sala na tafakari

.“Muda huu wa Ijumaa Kuu ni wa kutafakari na kujitathmini. Suluhisho la matatizo yetu lipo kwa Mungu,” alisema.

Askofu wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki ya Eldoret, Dominic Kimengich, alisema ushuru wa juu, umasikini, ukandamizaji na tamaa ya pesa ndivyo vinavyowasukuma watu wengi kuingia kwenye biashara haramu ya viungo vya binadamu.

“Tamaa ya fedha inaharibu nchi yetu, na huo sio mwelekeo tunaopaswa kuchukua. Mungu anataka taifa lenye amani na umoja, ambapo kila mtu anaheshimiwa ,” alisema Askofu Kimengich.

Askofu Benjamin Tarus wa Kanisa la African Inland Church (AIC) eneo la Kitale aliwahimiza Wakenya kuzingatia ustawi wao na kufanya kazi kwa bidii kusaidia familia zao.

“Tunaomba amani na mshikamano. Tunaomba viongozi wa kisiasa waheshimiane na wawe waangalifu na lugha wanayotumia katika majukwaa ya umma,” alisema Askofu Tarus.