Habari za Kitaifa

Viongozi wa Kirinyaga walaani utekaji nyara wa vijana

Na   GEORGE MUNENE December 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI kadhaa kutoka Kaunti ya Kirinyga wamelalamikia ongezeko la visa vya utekaji nyara wa vijana nchini.

Wakiongozwa na Seneta Kamau Murango, viongozi hao walisisitiza kuwa visa hivyo vinatisha kwa sababu wahusika katika utekaji nyara huo hawajulikani.

Seneta huyo ameitaka serikali kuwatambua wanaowateka nyara vijana hao na malengo yao.

“Watoto wetu waachwe. Wakitaka kunikamata wafanye hivyo lakini waache watoto wetu,” akasema Seneta Murango.

Kwa upande wake, Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga Njeri Maina alisema kuwa maelezo kwenye akaunti za mitando ya X na Facebook ya vijana hao yamefutwa.

Mbunge huyo aliitaka serikali kuamuru kuachiliwa huru kwa vijana hao au wawasilishwe kortini ili washtakiwe kwa mujibu wa sheria.

“Wazazi ambao watoto wao wametekwa nyara wanahisi machungu. Ikiwa ni serikali imewaweka mateka, basi iwaachilie huru,” Bi Maina akasema, akiahidi kuwatetea kortini.

Mbunge huyo ni Wakili.

Wakiongea katika eneo la Kibingoti, eneobunge la Ndia, viongozi hao walitaja visa viwili ambapo vijana wawili, Billy Munyiri Mwangi 24 na Peter Muteti, 22, walitekwa nyara Jumamosi, Desemba 21, 2024.

Kufikia leo, Jumanne, Desemba 24 hawakuwa wamepatikana.

Mwangi, ambaye ni mwanafunzi katika chuo kimoja cha kadri, alikuwa katika kinyozi, akisubiri zamu ya kunyolewa allipotekwa nyara.

Hapo ndipo gari jeupe lilifika na kumchukua kwa nguvu huku watu waliokuwa eneo hilo wakitazama kwa mshangao.

Bw Mwangi alipotaka kujua ni kwa nini alikuwa akikamatwa, wanaume hao wanne walijibu; “Utajua baadaye.”

Kulingana na familia, mwana wao alitekwa nyara Jumamosi mwendo wa saa tisa alasiri.

“Mwana wetu alikuwa katika duka la kinyozi akisubiri zamu yake anyolewe na ghafla wanaume hao wakafika na kumchukua bila kutoa sababu zozote,” akasema Bi Regina Wairimu, mamake Mwangi.

Bi Wairimu alisema alipokea habari kwamba mwanawe alikamatwa na kupelekwa kusikojulikana.

“Bado tumepigwa na mshangao kufuatia kile kilichomtendekea mwana wetu. Ikiwa serikali ndio ilihusika namtaka mtoto wangu akiwa hai. Na ikiwa mtoto wangu ametenda kosa lolote niko tayari kuomba msamaha kwa niaba yake,” Bi Wairimu akasema huku akitokwa na machozi.

Gerald Karicha, babake Bw Mwangi pia amezongwa na machungu kufuatia kutekwa nyara kwa mwanawe.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga