Viongozi waanza kumezea mate viatu vya Raila anayehemea kiti cha bara Afrika
NA JUSTUS OCHIENG
HUENDA hatua ya kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, kutangaza nia ya kuwania uenyekiti katika Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), ikazua makabiliano makali ya uongozi katika ODM na Azimio la Umoja.
Ijapokuwa Bw Odinga hajatangaza atakuwepo kumuunga mkono yule atahitaji uungwaji mkono wake, wadhifa huo huwa una majukumu mengi sana.
Nafasi hiyo ina majukumu mengi na mazito kuliko ile ya Mwakilishi Mkuu wa Muungano wa Afrika (AU) kuhusu Ustawishaji wa Miundomsingi, aliyoishikilia hapo awali.
Tayari, Bw Odinga amesema kuwa chama chake cha ODM na muungano wa Azimio una viongozi wafaao kuziongoza, hata ikiwa atazidiwa na majukumu kama mwenyekiti wa AUC. Hilo ni ikiwa atafanikiwa kuchaguliwa kuhudumu katika nafasi hiyo.
“Uongozi wa kisiasa huwa umegawanywa. Hata ikiwa sitakuwepo, kuna watu wenye uwezo karibu nami, walio tayari kuchukua uongozi katika ODM na Azimio,” akasema Bw Odinga kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Ikizingatiwa ODM ina manaibu wawili wa viongozi wa chama—magavana wa zamani Hassan Joho (Mombasa) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) mtawalia—si wazi kuhusu yule, baina ya viongozi hao wawili, anayeweza kuchukua nafasi ya Bw Odinga, ikiwa kigogo huyo atajiondoa katika nafasi yake, kuangazia majukumu mapya katika AUC.
Katika Azimio la Umoja, ijapokuwa kiongozi za Narc Kenya, Bi Martha Karua alikuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga kwenye uchaguzi uliopita, kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, anaonekana kuchukua uongozi wa mrengo huo na kuzindua kampeni za kuwania urais 2027.
Tayari, Bw Musyoka ashaungana na kiongozi wa chama cha DAP-K, Eugene Wamalwa, anayeonekana kuwa mgombea-mwenza wake, ambapo washaanza kampeni kali kote nchini.
Hata hivyo, vigogo wote katika muungano huo wamemuunga mkono Bw Odinga kuwania uenyekiti katika AUC.
Katika ODM, Bw Joho alirejea kwenye ulingo wa siasa wiki iliyopita, na kutangaza nia ya kuwania urais 2027 kwa tiketi ya chama hicho. Alitangaza kivumbi kikali baina yake na Bw Oparanya kupigania tiketi ya chama hicho.
“Nimemalizana na siasa za Mombasa. Nitawania nafasi ya urais. Nimesikia baadhi ya watu wakisema watawania urais; ningetaka pia kuwaambia kwamba nitakuwa kwenye kinyang’anyiro hicho,” akasema Bw Joho.
Akaongeza: “Katika chama cha ODM, kuna kiongozi wa chama na manaibu viongozi wa chama—mimi na Bw Oparanya. Yeye [Oparanya] pia analenga kuwania urais. Ningetaka kumwambia tutapigania tiketi hiyo katika ODM.”
Bw Joho alimrai Bw Odinga kumuunga mkono, kama vile alivyomuunga mkono Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki mnamo 2002 kupitia kauli “Kibaki Tosha”.
Mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho, Bw John Mbadi, alisema kuwa Kamati Kuu ya Chama itakutana hivi karibuni, baada ya Bw Odinga kurejea nchini kutoka Ujerumani, ili kutathmini mustakabali wa chama hicho.
“Baada ya Bw Odinga kurejea nchini kutoka Ujerumani, tutaketi chini kama Kamati Kuu na kutoa tangazo kuhusu mustakabali wa ODM. Ningetaka kuwaambia kwamba hakuna sababu yoyote kuwepo kwa wasiwasi,” akasema Bw Mbadi.
Akihutubu katika eneobunge la Suna Mashariki, alikokuwa amealikwa na mbunge Junet Mohamed—aliye pia Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa—Bw Mbadi alisisitiza kuwa “kiongozi wa ODM ni Raila Odinga, bila kujali ikiwa ndiye atakuwa mwenyekiti wa AUC au la”.
Akimtaja Bw Odinga kuwa twiga kisiasa, Bw Mohamed aliwaambia wale ambao wameanza kuwa na wasiwasi kutokuwa na hofu yoyote.
Licha ya hakikisho hizo, mbunge mmoja aliiambia Taifa Leo kuwa tayari, kuna makundi ambayo yameanza kuibuka katika chama hicho, yakiwa tayari kupigania uongozi wake, ikiwa Bw Odinga atachaguliwa katika nafasi hiyo.
“Ninawahakikishia mtarajie makabiliano makali katika kambi zinazoegemea mirengo ya Bw Joho au Bw Oparanya. Unakomwona Junet, jua kwamba hiyo ni kambi ya Bw Joho. Makabiliano hayo yataendelea,” akasema mbunge huyo.
Mdadisi wa siasa, Prof Macharia Munene, anasema kuwa tangazo la Bw Odinga kuwania nafasi hiyo halitaathiri sana siasa hapa nchini.
“Ushawishi wake utaendelea kama kawaida, kama ilivyokuwa alipohudumu kama Mwakilishi Mkuu wa AU wa Ustawishaji wa Miundomsingi. Ikiwa atapata kazi hiyo au la, ataendelea kuwa mgombea urais wa 2027 na miaka ijayo. Rais Ruto angependa kumwondoa kwenye ulingo wa siasa nchini, japo hilo halitafaulu,” akasema Prof Munene.