Habari za Kitaifa

Viongozi wataka majani ya muguka yatajwe dawa ya kulevya

June 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

CECIL ODONGO Na KEVIN CHERUIYOT

BAADHI ya viongozi wa kisiasa na kijamii Jumanne walitoa wito kuwe na mabadiko kwenye Sheria ya Mimea ya 2013 na Mwongozo wa Miraa 2023 kuondoa muguka kama mmea wa mavuno.

Viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi wamesema kuwa muguka ni dawa ya kulevya na ina kemikali ambayo Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (Nacada) imesema ni hatari kwa binadamu.

“Kemikali hizo cathinone na cathine ni hatari ndiposa Muguka imepigwa marufuku kwenye mataifa mengi ya Ulaya, eneo la Gulf kisha Tanzania na Uganda,” akasema Bw Mwinyi.

Muguka ambayo ni aina ya miraa imeorodheshwa kama mmea katika Kifungu cha Sheria za Mimea za 2013 na Mwongozo wa Sekta ya Kilimo cha Miraa 2023.

Bw Mwinyi alisema athari mbaya za kiafya zilizoko kwa watumiaji wa Muguka ni wazi na lazima kuwe na sheria ya kuiharamisha nchini.

Alikuwa akiongea Jumanne katika Msikiti wa Jamia jijini Nairobi ambapo viongozi wa kisiasa, wasomi na wataalamu kuhusu masuala ya afya na kiakili kutoka umma wa Kiislamu walikongamano kuzungumzia athari hasi za muguka.

Viongozi hao walitoka kaunti za Pwani na Kaskazini Mashariki. Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Mombasa Zamzam Mohamed, wawakilishi kutoka kamati ya Msikiti wa Jamia, Baraza Kuu la Waislamu na Shirika la Maahad Da’wah pia walikuwepo.

Marufuku

Mwezi Mei kaunti za Mombasa, Kwale, Kilifi, Lamu na Taita Taveta zilipiga marufuku muguka zikisema ina athari sana katika afya ya kiakli ya vijana kutoka eneo hilo.

Bw Mwinyi ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya ODM pia aliishambulia serikali kutokana na undumakuwili wake kuhusu mjadala unaoendelea kuhusu marufuku ya miraa.

Mbunge huyo alimtaka Naibu Rais Rigathi Gachagua atumie nguvu na juhudi kuhakikisha Muguka inatokomezwa Pwani, jinsi alivyoendeleza vita dhidi ya pombe haramu eneo la Kati mwa Kenya.

“Serikali inazingatia sana manufaa ya kiuchumi kwa wakulima wa Muguka na kupuuza athari za kiafya kwa wale ambao wanatumia mmea huo.

“Ni kinaya kuwa kwa upande moja Bw Gachagua yupo mstari wa mbele wa kupigana dhidi ya pombe haramu eneo la Mlima Kenya ilhali amelipa kisogo suala la Muguka maeneo mengine,” akasema Bw Mwinyi.

Bi Zamzam naye alisema soko la Miraa na Muguka linaendelea kudidimia hata katika mataifa ya nje na serikali inastahili kuwasaidia wakulima wa mimea hiyo wakumbatie aina nyingine ya kilimo.

Aliongeza kuwa muguka ni tishio kwa kizazi kijacho kwa sababu imewasababishia vijana msongo wa mawazo, kusambaratisha ndoa zao na pia kupungua kwa mbegu za uzazi.

“Suluhu ni serikali iwarai wakazi wakumbatie kilimo cha mimea mingine badala ya Miraa na Muguka. Tunaunga mkono juhudi za kuharamisha Miraa na Muguka kama mimea,” akasema Bi Mohammed.