Habari za Kitaifa

Vyama 48 vya kisiasa kugawana Sh2 bilioni

March 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA DAVID MWERE

JUMLA ya vyama 48 vya kisiasa vimetengewa kitita cha Sh2 bilioni katika mwaka ujao wa kifedha kulingana na ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti (BAC) kuhusu Taarifa ya Sera kuhusu Bejeti (BPS) iliyopitishwa bungeni wiki jana.

Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu alikuwa ameitisha mgao wa Sh6 bilioni kwa vyama hivyo katika mwaka huo wa kifedha wa 2024/2025 unaoanza Julai 1, mwaka huu.

Kupitishwa kwa BPS sasa kunaweka msingi wa kuandaliwa kwa makadirio ya bajeti ya kitaifa ambayo yatawasilishwa bungeni kabla ya Aprili 30 miaka miwili kabla ya kutamatika kwa mwaka huu wa kifedha.

Pesa hizo, Sh2 bilioni zilizotengewa vyama vya kisiasa zitagawanywa kwa vyama hivyo kwa misingi ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Hata hivyo, huenda mgao huo ukaongezwa au kupunguzwa kwa sababu mchakato wa utayarishaji wa bajeti ya kitaifa ungali unaendelea.

Kupungua au kuongezwa kwa mgao huo kutategemea shughuli ambazo serikali itazipa kipaumbele katika mipango yake ya matumizi ya fedha katika mwaka ujao wa kifedha.

Bi Nderitu anaamini kuwa vyama vya kisiasa vitatengewa kiasi hicho cha fedha ikizingatiwa vinatekeleza mchango mkubwa katika uongozi wa kidemokrasia nchini.

“Baada ya mgao huu wa fedha kuidhinishwa na bunge, Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa itakadiria na kuweka wazi kiasi cha fedha ambazo zitaelekezwa kwa Hazina ya Vyama vya Kisiasi na kile ambacho kila chama cha kisiasa kitapokea kama mgao,” akasema Bi Nderitu.

Chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Rais William Ruto kilichoko na jumla ya wabunge 145 kinatarajiwa kupata mgao mkubwa, kikifuatiwa na kile cha ODM chenye wabunge 86.

Nambari tatu katika usanjari huo ni chama cha Jubilee chake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta chenye wabunge 28 katika bunge la kitaifa.

Chama cha Wiper, chake makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka kinafuatia kwa wabunge 26 huku Ford Kenya chake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kikiwa na wabunge sita pekee ishara kwamba kitapokea mgao mdogo wa fedha hizo.

Chama cha The Servic Party (TSP) chama Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri chenye wabunge wawili pekee pia kiko katika tapo hilo.

Kulingana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2022, vyama vya kisiasa ambavyo vilishinda angalau kiti kimoja cha udiwani vinahitimu kupokea mgao wa fedha kutoka Hazina ya Vyama vya Kisiasa.

Hata hivyo, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna analalamika kuwa Sh2 bilioni zilizotengewa vyama vya kisiasa ni finyu, hali inayoashiria kuwa serikali inalenga kulemaza demokrasia ya vyama vingi.

“Tunafahamu kuwa wanalenga kuhujumu demokrasia ya vyama vingi matumaini potovu ya kurejesha taifa hili katika udikteta wa utawala wa chama kimoja. Hili haliwezi kufanyika nyakati kama hizi,” akasema.

Kulingana na Sehemu ya 24 ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2022, asilimia 0.3 ya mapato ya serikali yaliyofanyiwa ukaguzi na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa yanapasa kugawiwa vyama vya kisiasa vilivyohitimu kwa msingi ya vigezo vilivyowekwa “na kwa matumizi yaliyoainishwa pekee.”

Kulingana na sheria ya sasa chama cha kisiasa hakiwezi kupata mgao wa fedha za Hazina ya Vyama vya Kisiasa ikiwa hakikushinda kiti chochote katika bunge la kitaifa, Seneti, mabunge ya kaunti na hakikushinda kiti chochote cha ugavana.

Aidha, chama cha kisiasa kitanyimwa ufadhili ikiwa zaidi ya thuluthi mbili ya maafisa wake ni wa jinsia moja na ikiwa hakina katika asasi zake za uongozi, mwakilishi kutoka makundi maalumu kama vile watu kutoka jamii zilizotengwa, wanawake na watu wanaoishi na ulemavu.