Waathiriwa Kwa Binzaro walizikwa kikatili kuliko Shakahola, wasema wachunguzi
Maafisa wa usalama walipomkamata mchungaji maarufu Paul Mackenzie pamoja na washirika wake 95 kufuatia vifo vya Shakahola vilivyohusisha zaidi ya maisha 450, msitu huo ukatangazwa kuwa mahali pa uhalifu na hadi sasa hakuna anayeruhusiwa kuingia humo.
Ili kuimarisha usalama msituni, kuna walinzi eneo hilo saa zote. Angalau maafisa 30 wako eneo hilo kila siku ili kuzuia watu kuingilia katika eneo ambalo wafuasi wa Mackenzie walizikwa katika makaburi baada ya kufa kwa njaa katika mfungo hatari.
Kulingana na serikali, hatua hizi zilichukuliwa ili kuzuia vifo vingine.
Hata hivyo, wakiwa na dhamira ya kuendelea kutenda uhalifu kwa jina la dini, wafuasi waliondoka msituni na kuhamia ndani zaidi katika msitu wa Chakama. Huko, walipata makazi mapya ya kuendeleza uharibifu, mara hii kwa mbinu mbaya zaidi.
Miaka miwili baadaye, tukio lingine jipya na la kusikitisha limeibuka katika kijiji cha Kwa Binzaro, takribani kilomita 27 kutoka Shakahola, ambapo mamia waliangamia kwa kufunga ili “kukutana na Yesu.”
Kwa Binzaro iko zaidi ya kilomita 30 kutoka kituo cha polisi kilicho karibu. Wananchi wanasema kutokuwepo kwa usalama au uwepo mdogo kabisa kumechangia sana shughuli za uhalifu zinazogunduliwa sasa msituni.
Serikali yenyewe imekubali kuwa ukubwa wa ranchi ya Chakama hufanya eneo hilo kuwa la shughuli haramu bila kutambuliwa.
Wakati huu, makaburi yamefichwa ndani ya vichaka na ni vigumu zaidi kugunduliwa. Fuvu na mabaki ya mifupa yanafukuliwa yakiwa yamesambaratika.
Wachunguzi wanasema wahalifu wamebadilisha mbinu. Tofauti na Shakahola, ambapo maiti nyingi ziliwekewa nguo, mashuka au blanketi, Kwa Binzaro, maiti zilizikwa bila nguo na uso ukiangalia juu.
Makaburi ni ya kina kifupi, karibu futi moja tu, kuonyesha wahalifu walikuwa na haraka kutupa maiti na kukimbia.
Katika baadhi ya matukio, mabaki ya mifupa yamekatika na kuoza na kuna harufu mbaya eneo hilo. Katika makaburi inaoneka waathiriwa waliandaliwa kabla ya mazishi.
Wale waliozoea maeneo yote mawili wanasema kuna tofauti kubwa. Wakati maiti za Shakahola zilifunikwa na mashuka au karatasi za nailoni, maiti za Kwa Binzaro zilikuwa zimetolewa nguo kabisa. Wachunguzi wanaeleza mazishi Kwa Binzaro ni ya kikatili zaidi.
Zaidi ya maiti zilizopatikana kwa sasa ni mifupa tu na zimechakaa vibaya. Wachunguzi wanaamini waathiriwa walizikwa angalau mwaka mmoja uliopita. Hii ina maana walikuwa hai wakati Mackenzie alipokamatwa 2023.
Hata hivyo, mazishi yanaonekana kufanana na ile ya Shakahola. Makaburi kadhaa yana maiti mbili au zaidi pamoja, zikiwa zimefunikwa kidogo sana na udongo. Tofauti na Shakahola, ambapo baadhi ya maiti zilikutwa chini ya kivuli cha miti, waathiriwa wote wa Kwa Binzaro walizikwa ndani ya vichaka.
Mpaka sasa, takriban maiti tisa zimefukuliwa Kwa Binzaro, kuongeza idadi ya Wakenya waliofariki kutokana na mafunzo hatari ya kidini hadi zaidi ya 470 tangu 2023, mwaka ambao makaburi ya kwanza yaligunduliwa Shakahola.