Wabunge kuamua hatima ya Linturi mnamo Mei 13
NA CHARLES WASONGA
WABUNGE sasa wataamua hatima ya Waziri wa Kilimo Mithika Linturi Jumatatu ijayo kwenye kikao maalum cha kujadili na kupigia kura ripoti ya Kamati Maalum iliyoteuliwa kuchunguza mashtaka dhidi yake.
Kwenya notisi kwa umma aliyoitoa Jumatatu, Mei 6, 2024, Bw Wetang’ula alisema kamati hiyo ya wanachama 11 inayoongozwa na naibu kiranja wa wengi Naomi Waqo, itawasilisha ripoti ya uchunguzi wake kuhusu uhalali wa madai yaliyoko kwenye hoja ya kumtimua Bw Linturi afisini kwa kuhusishwa na sakata ya mbolea feki.
Hoja hiyo ambayo imedhaminiwa na Mbunge wa Bumula Jack Wamboka, ilipitishwa na wabunge 149 na 36 wakapinga mnamo Alhamisi, Mei 2, 2024.
“Sasa notisi inatolewa kwa wabunge wote wa Bunge la Kitaifa na umma kwamba, kwa mujibu wa Kipengele cha 152 (7) (b) cha Katiba na Sheria za Bunge 64 (3) na 66, nimeteua Jumatatu, Mei 13, 2024 saa nane na nusu kama siku na saa ya kikao maalum cha kupokea ripoti ya Kamati Teule,” akasema Bw Wetang’ula katika tangazo hilo.
Wanachama wa Kamati hiyo waliteuliwa Alhamisi wiki jana saa chache baada ya wabunge kupitisha hoja hiyo na wakapewa muda wa siku 10 kuchunguza madai dhidi ya Bw Linturi kwa lengo la kubaini ikiwa yamefafanuliwa ipasavyo au la.
Kando na Bi Waqo, ambaye ni Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Marsabiti (UDA) wanachama wengine wa kamati hiyo ni Bw Robert Mbui (Kathiani, Wiper), Rachael Nyamai (Kitui Kusini, Jubilee), Samuel Chepkonga (Ainabkoi, UDA), George Murungara (Tharaka, UDA), TJ Kajwang (Ruaraka, ODM), na Moses Injendi.
Wengine ni Jane Njeri Maina (Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga, UDA), Kassim Tandaza (Matuga, ANC), Catherine Omanyo (Busia, ODM) na mbunge wa Wajir Magharibi Yusuf Farah (ODM).
Katika hoja yake Bw Wamboka anamtuhumu waziri Linturi kwa makosa kama vile Ukiukaji wa Katiba na sheria nyingine, uhalifu chini ya sheria ya kitaifa na mienendo mibaya isiyokubalika kwa afisa wa hadhi yake.
Madai dhidi ya Bw Linturi yanahusu ununuzi na usambaji wa mbolea ya ruzuku iliyonunuliwa na serikali kisha kukatokea ripoti kuwa baadhi ya mbolea hizo zilikuwa feki.
Ikiwa kamati hiyo teule itagundua kuwa tuhuma hizo hazijafafanuliwa, bunge litakomesha mchakato wa kumtimua Bw Linturi.
Lakini ikiwa kamati ya Bi Waqo itagundua kuwa madai hayo yamefafanuliwa ipasavyo, Bunge la Kitaifa litampa Bw Linturi nafasi ya kujitetea kabla ya kuipigia kura.
Ikiwa ripoti ya kamati hiyo itaungwa mkono na angalau wabunge 176, spika Wetang’ula atawasilisha ripoti kwa Rais William Ruto na pendekezo kwamba amfute kazi Bw Linturi.