Wabunge kuandaa kikao kupanga ajenda ya 2026
Maandalizi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, pamoja na changamoto zinazokumba utekelezaji wa mfumo wa Elimu unaozingatia Umilisi (CBE), ni miongoni mwa ajenda kuu zitakazojadiliwa wabunge watakapokutana Naivasha kuanzia Jumatatu.
Wabunge wote wa Bunge la Kitaifa watakutana Naivasha kwa mkutano wao wa kila mwaka, ambao pia utajadili mustakabali wa Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) kabla ya kufunguliwa tena kwa Bunge Februari 10, 2026.
Mbali na masuala ya uchaguzi na mpito wa wanafunzi kujiunga na Sekondari Pevu hususan Gredi 10 ya kwanza chini ya CBE, wabunge pia watakutana na Waziri wa Fedha John Mbadi na mwenzake wa Afya, Aden Duale, kujadili hali ya uchumi na utoaji wa huduma za afya nchini.
“Huku nchi ikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu ujao, mfumo wa kisheria na kifedha unaosimamia vyama vya kisiasa unahitaji kuangaziwa upya na Bunge ili kulinda uaminifu wa uchaguzi, haki na uthabiti wa kisiasa,” unasema waraka utakaongoza mkutano huo.
Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, anatarajiwa kufika mbele ya wabunge Jumanne ili kuwapa tathmini ya maandalizi ya tume hiyo katika kuendesha uchaguzi wa kuaminika mwaka 2027.
“Mkutano huu utawapa wabunge fursa ya kuhoji IEBC na taasisi nyingine husika, kwa kuzingatia hali ya mipaka ya uchaguzi, usajili na elimu ya wapigakura, teknolojia ya uchaguzi, na mifumo ya kisheria na sera,” Bunge limesema.
Kuhusu utekelezaji wa CBE, Waziri wa Elimu Julius Ogamba atafika mbele ya wabunge Jumatano kueleza wasiwasi mkubwa miongoni mwa wadau wa elimu, hasa kuhusu miundombinu ya shule, maandalizi ya walimu, ufadhili na uwiano wa walimu kwa wanafunzi kadri wanafunzi wanavyopanda madarasa.
Bw Ogamba atazungumzia mada ya ‘Mpito kutoka Sekondari Msingi hadi Sekondari Pevu, Ufadhili, Ujenzi wa Miundombinu ya Shule na Maandalizi ya Walimu’.
“Kikao hiki kitawapa wabunge fursa ya kutathmini hali ya sasa ya utekelezaji wa CBE na kuangalia hali ya taasisi za serikali kushughulikia changamoto hizi, kwa lengo la kubaini hatua za sera na kisheria za kuimarisha utekelezaji endelevu wa mtaala,” Bunge limesema.
Kuhusu hali ya uchumi, Bw Mbadi atawafahamisha wabunge kuhusu mazingira ya sasa ya kiuchumi huku kukiwa na shinikizo la bajeti na ongezeko la mahitaji ya huduma za umma.
Majadiliano hayo yatakayofanyika katika wakati muhimu wa Bunge la sasa pia yatatoa fursa ya kutathmini hatua zilizopigwa hadi sasa na kuzingatia hatua za sera au sheria zinazohitajika kuunga mkono Hazina ya Kitaifa.
Mazungumzo kati ya wabunge na Bw Mbadi yatachangia mageuzi ya bajeti na sera za kifedha yanayolenga kushughulikia changamoto za utekelezaji na kuimarisha matokeo katika mwaka wa kifedha wa 2026/2027.
Katika kikao hicho, wabunge pia watapitia utekelezaji wa Bajeti ya 2025/2026, kubaini changamoto na mafunzo yaliyopatikana, na kutumia taarifa hizo kwa maandalizi ya Bajeti ya 2026/2027.
Kuhusu Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Bw Duale atakabiliwa na maswali ya wabunge kuhusu hali ya sekta ya afya, hasa utoaji wa huduma chini ya SHA katika usimamizi wa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).
Bw Duale anatarajiwa kuwapa wabunge taarifa kuhusu hali ya mageuzi muhimu ya sekta ya afya yanayoendeshwa na Wizara ya Afya na kutathmini changamoto zinazoathiri upatikanaji, ubora, gharama nafuu na usawa wa huduma za afya.
Wabunge pia watakutana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa, John Cox Lorionokou, kuangazia mfumo wa kisheria na udhibiti wa vyama vya kisiasa, hususan ufadhili wa vyama.
Kikao hicho kitachunguza iwapo sheria zilizopo zinatosha kukuza demokrasia ya ndani ya vyama, ushindani wa haki, uwazi na uwajibikaji, huku zikikuza mazingira jumuishi ya kidemokrasia.
Kuhusu NG-CDF, wabunge watachunguza chaguo zote za kisheria huku wakisubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuhusu uhalali wa mfuko huo.
Mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo, anatarajiwa kuwafahamisha wabunge kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa, ikiwemo chaguo za kisheria, sera na kiutawala, ili kulinda mafanikio ya maendeleo, kuhakikisha uzingatiaji wa Katiba, kuimarisha uwajibikaji na kutoa mwelekeo wa baadaye wa miradi ya maendeleo ya maeneo bunge.