Habari za Kitaifa

Wabunge kutoa heshima zao kwa marehemu Jenerali Ogolla

April 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa Jumatano litafanya kikao maalum cha kutoa heshima kwa marehemu Mkuu wa Majeshi (CDF) Jenerali Francis Ogolla na wanajeshi wengine tisa waliokufa katika ajali ya helikopta Alhamisi wiki jana.

Kwenye taarifa aliyowasilisha Jumanne katika kikao cha alasiri, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alisema kuwa wakati wa kikao hicho, hoja inayopendekeza maafisa wa KDF na vikosi maalum kupewa kipaumbele na mashirika ya ndege itajadiliwa.

Hoja hiyo ambayo imedhaminiwa na Mbunge wa Lamu Mashariki Ruweida Obo, iliwasilishwa bungeni mara ya kwanza Oktoba 2023.

“Nafasi itatolewa kwa Mheshimiwa Obo kuwasilisha rasmi hoja yake huku wabunge wakipewa nafasi kutoa heshima zao kwa marehemu Jenerali Ogolla na kutambua mchango wa KDF katika kulinda mipaka ya Kenya,” Bw Wetang’ula akasema.

Wakati wa kikao cha Jumanne, Spika huyo pia aliwaongozA wabunge kutulia kwa dakika moja kwa heshima Jenerali Ogolla na wanajeshi tisa walioangamia pamoja naye katika ajali hiyo.

Waliaga dunia baada ya helikopta iliyokuwa ikiwasafirisha kuanguka na kuteketea katika kijiji cha Sindar, kata ya Tot, kwenye mpaka wa kaunti za Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi.

Bw Wetang’ula pia alitumia nafasi hiyo kutoa ujumbe wa heri njema na kuwatakia afueni wanajeshi wawili walionusurika katika ajali hiyo, ya kwanza nchini kuhusisha helikopta iliyombeba Mkuu wa Majeshi.

Wabunge nao walitumia fursa hiyo kutoa rambirambi zao kwa familia za Jenerali Ogolla na wanajeshi wengine tisa walioangamia.

Miongoni mwa wabunge waliopata nafasi ya kutoa rambirambi zao ni kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah, kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi na wabunge Omboko Milemba (Emuhaya), Geoffrey Ruku (Mbeere Kaskazini), Raphael Wanjala (Budalang’i), na Samuel Atandi (Alego Usonga) miongoni mwa wengine.

Wabunge hao wote walitaka uchunguzi wa kina ufanywe kubaini chanzo cha ajali hiyo huku wakitaka Jeshi la Ulinzi la Kenya liongezewe mgao wa fedha ili liweze kununua ndege mpya na salama za usafiri.

Jenerali Ogolla alizikwa Jumapili nyumbani kwake katika eneo la Ng’iya, Kaunti ya Siaya katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Rais William Ruto na wageni kutoka nchini na mataifa ya kigeni.

Katika hoja yake, Bi Obo ambaye ni rubani, anaitaka Wizara ya Uchukuzi kuanzisha kanuni ya kuabiri ndege ambapo wanajeshi wa sasa na wastaafu watapewa kipaumbele kuabiri kabla ya raia.

Mbunge huyo wa Lamu Mashariki anasema kuwa wanajeshi hutekeleza wajibu mkubwa wa kulinda usalama wa kitaifa na hadhi kama hiyo ndio mojawapo ya njia za kutambua mchango huo.

“Ni muhimu kuwapa wanajeshi wetu hadhi na heshima sawa na inavyofanyika katika nchi nyingine ambako maafisa hao wanapewa kipaumbele mbele ya raia wengine katika benki na wakati wa kuabiri ndege,” akasema Bi Obo.

Alisema kuwa hadhi kama hiyo itawaongezea fahari na kuwaongeza moyo wanapotekeleza majukumu yao ya kudumisha usalama wa kitaifa.

Mbunge huyo alisema mataifa kama vile Amerika na Uingereza yameweka sera ambapo wanajeshi wanaohudumu na wale waliostaafu wanapewa kipaumbele katika viwanja vya ndege.