Wabunge, maseneta waonyesha hasira za wazi kwa Rais zogo la ufisadi likitishia kuwa baya
WABUNGE na maseneta walionyesha hasira za wazi kufuatia kauli ya Rais William Ruto ya kuwahusisha na ufisadi na wakasusia kikao walichopanga kujadili miswada muhimu ya serikali jana asubuhi.
Bunge la Kitaifa lilikatiza kikao chake cha asubuhi kwa kukosa idadi ya kutosha ya wabunge, licha ya kuwa na ajenda muhimu za serikali huku wachanganuzi wakisema hatua hiyo ya wabunge inaweza kuwa ni njia ya kulalamika baada ya Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwashutumu vikali kwa madai ya kushiriki ufisadi.
Kwa mujibu wa kalenda ya Bunge la Kitaifa, kila Jumanne, wabunge hukutana saa nane na nusu alasiri kwenye kikao kikuu, huku asubuhi ikiwa imehifadhiwa kwa shughuli za kamati.
Hata hivyo, wiki iliyopita Bunge lilipitisha azimio la kufanya kikao cha dharura jana asubuhi, ili kukamilisha shughuli muhimu za serikali kabla ya kuanza likizo ndefu inayopangwa kuanza leo Agosti 20, 2025.
Lakini kufikia wakati Naibu Spika Gladys Boss aliingia ukumbi wa mjadala, ni takribani wabunge watatu pekee waliokuwepo.
Kwa mujibu wa Katiba, angalau wabunge 50 kati ya 349 wanapaswa kuwa ndani ya ukumbi ili Bunge lifanye kazi kwa mujibu wa sheria.
“Kwa kuwa hakuna idadi ya kutosha ya wabunge, Bunge limeahirishwa hadi saa nane na nusu alasiri,” Bi Boss alitangaza.
Katika kikao cha alasiri, wabunge wa pande zote walikosoa vikali kauli ya rais na hata kuwataka maspika wa seneti na Bunge la Kitaifa Amason Kingi na Moses Wetang’ula kumwamuru Rais Ruto kuwasilisha ushahidi alio nao kuhusu kuhusika kwao na ufisadi.
Wabunge hao walitishia kuwatimua maspika hao iwapo hawatamuita kiongozi wa nchi kufika mbele yao kutoa ushahidi huo.
“Spika Wetang’ula na Kingi, ninyi ndio wakuu wa taasisi hii, lazima mtekeleze Kifungu cha 125 na kumwita Rais. Kifungu hicho hakimkingi Rais. Kinasema kuwa Bunge lina mamlaka ya kumwita mtu yeyote,” alisema Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’.
“Wacha Rais afike mbele ya kamati ya Bunge na kurudia kile amekuwa akisema katika mikutano ya hadhara. Alete ushahidi ili ushughulikiwe kwa mujibu wa sheria. Maspika hao wawili lazima wasimame kidete,” aliongeza.
Katika mkutano wa kwanza wa pamoja wa Kenya Kwanza na ODM uliojumuisha maseneta Jumatatu, Rais Ruto alisema wabunge wanaochukua rushwa watashtakiwa badala ya kuaibishwa tu.
Vilevile, Bw Odinga alidai kuwa wabunge hawapaswi kusimamia Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF), akiongeza kuwa baadhi yao wanatumia vibaya madaraka yao.
Jana, alasiri wakiongozwa na viongozi wa wengi na wachache Kimani Ichungwah na Junet Mohamed, wabunge walikosoa vikali kauli za vinara hao wawili wa Serikali Jumuishi kwa kupaka tope uadilifu wao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki na Masuala ya Kisheria, George Gitonga Muragura, alikanusha madai kwamba, kamati hiyo na wanachama wake walipokea hongo ya Sh10 milioni wakati wa kuzingatia Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Kupambana na Ulanguzi wa Pesa Haramu 2025.
“Kwa niaba ya Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria, ningependa kusema kwa uwazi kabisa kuwa, kamati haikuomba wala haikupokea kishawishi cha aina yoyote kutoka kwa mtu yeyote au upande wowote wakati wa kuzingatia Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Kupambana na Ulanguzi wa Pesa 2025, kama inavyodaiwa,” alisema Mbunge huyo.
Mbunge wa Rarieda Otiende Omollo alisema Rais aliwakosea wabunge heshima kwa kudai ni wafisadi.
“Baadhi yetu tuko na jina la kulinda nje ya bunge na mtu anaposema sisi ni wafisadi anatudunisha,” alisema.
Naye mbunge wa Bumula alidai Rais alikasirishwa na wabunge kwa kuwa walianika uozo katika e-Citizen.
Miswada miwili iliyowasilishwa kwa niaba ya serikali na Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah (Mbunge wa Kikuyu) ilipangiwa kujadiliwa katika hatua ya kamati ya Bunge zima, ambapo kazi halisi ya kutunga sheria hufanyika lakini Bw Ichung’wah hakuwa bungeni wakati wa kikao cha asubuhi.
Pia, kulikuwa na Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uhalifu wa Kidijitali na Matumizi Mabaya ya Kompyuta (2025), ambapo kura ya mwisho ilipaswa kupigwa.
Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mawakili (2025) nao ulipaswa kujadiliwa kupitia Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria inayoongozwa na Mbunge wa Tharaka, Gitonga Murugara ambaye pia alisusia kikao.
Mswada mwingine ni wa Marekebisho ya Sheria ya Barabara (2025), uliodhaminiwa na Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma ambao ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya pili.
Lakini Kaluma pia hakuhudhuria. Kamati ya Utalii na Wanyamapori inayoongozwa na Mbunge wa Maara Kareke Mbiuki ilikuwa ipitie taarifa ya wizara kuhusu migogoro ya mara kwa mara kati ya binadamu na wanyama katika maeneo ya Igembe North, Chepalungu na Aldai, kupotea kwa mvuvi Brian Makori Odhiambo kutoka Nakuru, kudorora kwa sekta ya utalii nchini na visa vya kuumwa na nyoka Baringo.
Wabunge walipokuwa wakionyesha hasira zao Rais William Ruto alizindua Jopokazi la Mashirika tofauti Kupambana na Ufisadi (MAT), hatua ambayo amesema italeta msukumo mpya katika vita vya serikali yake dhidi ya ufisadi.
Kupitia Amri ya Rais ya kwanza mwaka 2025, Dkt Ruto alianzisha rasmi jopo hilo chini ya Idara ya Serikali ya Haki, Haki za Kibinadamu na Masuala ya Katiba.
Mashirika hayo ni pamoja na; Afisi ya Rais ambayo itakuwa mwenyekiti wa jopo, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye atahudumu kama katibu wake.
Mashirika mengine ni; Idara ya Ujasusi wa Kitaifa (NIS), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Afisi ya DPP, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), kati ya asasi nyingine.
Ripoti za DAVID MWERE, EDWIN MUTAI, JUSTUS OCHIENG, BENSON MATHEKA