Wabunge nao wataka usemi katika kuajiri wazee wa vijiji
Juhudi za wabunge kutaka washirikishwe katika uteuzi wa wazee wa vijiji, wanavyoajiriwa na malipo yao zimeibua vita vya kudhibiti maafisa 106,000 wanaohudumu mashinani, huku umuhimu wao ukitarajiwa kuongezeka Kenya inapoelekea uchaguzi mkuu wa Agosti mwakani.
Ni miezi mitatu tu tangu wazee hao waanze kupokea posho ya Sh3,000 kila mwezi, lakini sasa wabunge wanadai kuwa watu waliokuwa wakihudumia jamii kwa muda mrefu bila malipo waliachwa nje ya orodha ya serikali.
Wanasema baadhi ya machifu na maafisa wa utawala walioshiriki kuwatambua wazee hao na kukusanya taarifa zao walipendelea jamaa na marafiki zao, badala ya kuwajumuisha wale waliokuwa wakifanya kazi hiyo kwa kujitolea.
Wabunge sasa wanataka Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kuwasilisha orodha ya wazee wote 106,000 wanaolipwa na serikali ili wahakikishe kuwa waliohudumia jamii kwa muda mrefu ndio wanaonufaika.
Suala hilo liliibuka Jumatano wakati wa kipindi cha maswali bungeni, ambapo mawaziri hujibu moja kwa moja maswali ya wabunge kuhusu shughuli za wizara zao.
Mwakilishi wa Wanawake wa Uasin Gishu Gladys Boss alisema mwanamke mzee aliyekuwa akihudumu Langas, katika kaunti hiyo, aliachwa nje ya orodha kwa sababu hakuwa na uhusiano mzuri na Kamishna wa Kaunti.
“Aliachwa nje kimakusudi kwa sababu Kamishna wa Kaunti hakumpenda. Hiki ni kisa kimoja tu; kuna visa vingi kama hivyo nchini,” alisema.
Alisema watu wengi walihudumu kama wazee wa vijiji kwa miaka mingi bila malipo, lakini serikali ilipoamua kuwalipa, wengine wapya walichukuliwa na kuwaondoa waliokuwa wamefanya kazi hiyo kwa uaminifu.
Mbunge wa Kajiado Kusini Samuel Parashina alitaka Waziri Murkomen kueleza vigezo vilivyotumiwa katika uteuzi huo.
Alisema baadhi ya machifu walichagua marafiki na jamaa zao, jambo linalozua maswali kuhusu haki na uwazi katika mchakato huo.
“Je, Waziri anaweza kuwasilisha ripoti kuhusu vigezo vilivyotumiwa kuwatambua wazee hawa? Je, kulikuwa na upendeleo? Na je, wale walioachwa nje licha ya kuhudumia jamii watapewa nafasi baadaye?” aliuliza.
Mbunge wa Igembe Kaskazini Julius Taitumu alisema wazee waliokuwa wakifanya kazi hiyo bila malipo ndio walioathirika zaidi baada ya serikali kutangaza posho.
Alisema machifu na manaibu wao walijikita katika kuchagua marafiki na watu wa ukoo wao walipotambua kuwa kazi hiyo sasa ingekuwa na malipo.
Akijibu wabunge, Bw Murkomen alisema serikali ilitarajia ushindani mkubwa wa kutaka kuwa mzee wa kijiji baada ya kuanzishwa kwa posho ya Sh3,000.
“Siku hizi imekuwa fahari kuwa mzee wa kijiji. Baadhi ya watu wanajitambulisha kama wazee wa vijiji; wengine ni wa kweli na wengine si wa kweli,” alisema.
Aliahidi kuwa wizara itatoa rekodi za wazee wote katika ofisi za makamishna wa kaunti kote nchini ili wananchi waweze kuthibitisha wanaostahili kupokea malipo hayo.
Alifichua kuwa kati ya wazee 106,000, huduma ya M-Pesa ya Safaricom ilikuwa imefanikiwa kushughulikia 96,566 na kuwalipa kupitia mfumo wa Tunza Vijiji.
Taarifa za waliobaki zilirudishwa kusahihishwa kwa kuwa majina hayakulingana na nambari za vitambulisho na simu.
“Usasishaji wa taarifa unaendelea na utakamilika ndani ya mwezi mmoja ili kuhakikisha wazee waliosalia wanalipwa posho zao kwa malimbikizi,” alisema.
Rais William Ruto alizindua sera ya usimamizi wa vijiji na utawala wa serikali ya kitaifa mwezi Agosti, hatua iliyowatambua rasmi wazee hao na kuwaingiza katika mfumo wa utawala wa kitaifa.
Serikali ilikusanya taarifa zao kote nchini na kuunda sajili ya kitaifa itakayotumiwa kuwatambua na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.
Rais alisema wazee hao ni kiungo muhimu kati ya serikali na wananchi kwa sababu wanafahamu changamoto za jamii na wako karibu na watu wanaohitaji huduma.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Kitaifa ya Watu na Makazi ya 2019, Kenya ilikuwa na kata 2,427 zinazosimamiwa na machifu na kata ndogo 6,612 chini ya manaibu wa machifu.
Hata hivyo, idadi ya kata imeongezeka hadi 2,735 na kata ndogo kufikia takriban 7,000.
Kwa sasa, mfumo huo una wazee wa vijiji 106,072, manaibu wa machifu 9,144 na machifu 4,008, wote wakiripoti kwa serikali ya kitaifa.
Serikali inataka kuwaunganisha wazee hao katika mfumo rasmi wa utawala, kuwapa majukumu yaliyo wazi na kuwawezesha kifedha ili kurahisisha utoaji huduma mashinani