Walimu walio na umri wa miaka 40 na zaidi waendelee kupuuzwa katika ajira ya TSC
Maelfu ya walimu waliohitimu mafunzo ambao hawakuajiriwa Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) wanahofia kufikisha umri wa kustaafu bila kupata nafasi ya kufundisha katika shule za umma.
Walimu walio na umri wa zaidi ya miaka 45 ndio walioathirika zaidi, huku baadhi yao wakilazimika kufanya kazi za vibarua, kufundisha katika shule za kibinafsi kwa mishahara midogo au kuacha kabisa ndoto ya kuwa walimu.
Hii ni licha ya serikali ya Rais William Ruto kuajiri zaidi ya walimu 100,000 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Walimu hao sasa wanangoja utekelezaji wa ahadi ya Rais ya kuwapa nafasi za ajira kupitia utaratibu maalumu wa kuwapa kipaumbele, aliyotoa alipokutana na walimu 10,000 katika Ikulu ya Nairobi Septemba 13, 2025.
Katibu Mkuu wa chama cha walimu wa shule za msingi KNUT, Collins Oyuu, alimuomba Rais kuwasaidia walimu wakongwe ambao wamekosa ajira huku wanaopaswa kuwa wanafunzi wao wakiajiriwa.
Mmoja wao ni James Cherop, mwenye umri wa miaka 52 kutoka Baringo, ambaye amesubiri ajira kwa miaka 24 tangu alipohitimu mafunzo mwaka 2002. Sasa anafanya vibarua katika Kaunti ya Nakuru ili kukimu familia yake ya watoto saba.
“Nimepoteza hesabu ya mara ambazo nimetuma maombi. Nilikata tamaa na kuamua kufanya kazi za mikono Nakuru ili kutunza familia yangu,” alisema.
Kenneth Rono, mwenye umri wa miaka 47 kutoka Bomet, pia amekuwa akifanya kazi za vibarua kwa miaka 10 bila kupata ajira ya TSC. Amefanya kazi za kupalilia, kuchuma majani ya chai, kuchimba vyoo na ujenzi.
Alisema shule ya kibinafsi aliyowahi kusomesha ilimlipa Sh7,000 pekee kwa mwezi, kiasi kisichotosha kutunza familia yake ya watoto wanne.
Walimu katika shule za kibinafsi hulipwa kati ya Sh6,000 na Sh8,000 kwa mwezi, ikilinganishwa na mshahara wa kuanzia wa Sh26,255 kwa walimu wa TSC. Pia hawana mafao kama pensheni, bima ya matibabu na malipo ya likizo.
Saddiq Hussein Mohamed, 51, kutoka Garissa, alihitimu Chuo cha Ualimu cha Garissa mwaka 1998. Alipata nafasi ya ajira lakini aliugua na kushindwa kuripoti kazini, na tangu wakati huo amekuwa akituma maombi bila mafanikio.
KNUT inataka nafasi za ajira zitengwe kwa walimu wenye umri wa miaka 45 na zaidi ili wasiendelee kuachwa nyuma.