• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Wabunge wa EALA nchini kupigia debe Raila

Wabunge wa EALA nchini kupigia debe Raila

NA VALENTINE OBARA

KAMPENI za kumtaka kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa mwenyekiti ajaye wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) zimezidi kupamba moto, huku wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Kenya wakilenga kusukuma azma yake mbele ya Bunge hilo.

Wabunge hao wa EALA kutoka Kenya wanataka kupata uungwaji mkono wa wenzao kutoka mataifa mengine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kushawishi mataifa yao kumuunga mkono Bw Odinga.

Kulingana na Mbunge wa EALA, Bw Hassan Omar, muhimu miongoni mwa mikakati yao itakuwa kumhitaji Waziri Mkuu huyo wa zamani awasilishe maono yake mbele ya Bunge hilo wakati wa vikao vyao nchini kuanzia wiki hii.

Wabunge hao ambao bunge lao liko jijini Arusha, Tanzania, walipangiwa kuwasili jijini Nairobi kuanzia jana, Jumapili, Machi 3 kwa ajili ya vikao vitakavyofanyika hadi Machi 20, 2024.

Bw Omar, mwanachama wa Chama tawala cha UDA, alisema kiongozi huyo wa ODM ndiye anafaa zaidi kwa nafasi hiyo kwa kuwa amekuwa akionyesha nia ya kupigania kuungana kwa bara la Afrika.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Wadi ya Junda, eneobunge la Kisauni mjini Mombasa Alhamisi iliyopita, alisema watataka Bw Odinga na Rais William Ruto watoe maoni yao binafsi na maono ya Kiafrika kwa wabunge wa EALA.

“Nitakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Raila, kama raia wa Afrika Mashariki anakuwa mwenyekiti wa AUC hivi karibuni,” alisema.

EALA ina wajumbe tisa waliochaguliwa kutoka kila moja ya nchi sita washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Wanachama wengine kutoka Kenya ni Suleiman Shahbal, Winnie Odinga, Kanini Kega, Kennedy Kalonzo Musyoka, Zipporah Kering, Iman Deko, Mwangi Maina na David Sankok.

Bw Shahbal awali alisema ananuia kuwasilisha hoja wakati wa kikao kijacho cha kuitaka EAC kuungana kuunga mkono azma ya Bw Odinga.

Kulingana na mwanasiasa huyo wa ODM, Bw Odinga amethibitisha kujitolea kwake kwa maendeleo ya bara Afrika na umoja.

“Raila Odinga ni mwanasiasa wa kweli wa Afrika Mashariki, ambaye uongozi wake na maono yake yameendeleza kwa kiasi kikubwa malengo yetu ya pamoja ya ushirikiano wa kikanda. Uhusiano wake wa muda mrefu na wakuu wa nchi katika bara zima unasisitiza uwezo wake wa kukuza ushirikiano na umoja,” alisema.

Kulingana na uamuzi wa 2018 wa Umoja wa Afrika, mwenyekiti wa tume ajaye anapaswa kutoka eneo la mashariki mwa Afrika.

Hata hivyo, Bw Odinga atalazimika kumenyana na wagombeaji wengine kadhaa ambao wanaweza kueleza nia yao ya kuwania kiti hicho.

Somalia ilimtangaza aliyekuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje Fawzia Adam kuwania kiti hicho kinachoshikiliwa na Moussa Faki Mahamat.

 

  • Tags

You can share this post!

Bonge la muungano wa Raila, Ruto na Mudavadi

CJ Koome alivyozima maandamano ya mawakili

T L