Wabunge waimba ‘Wan Tam’ mbele ya Ruto wakikasirikia ‘kugombezwa kama watoto’
RAIS William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga walizomewa na wabunge, baadhi wakiimba ‘Wan Tam’ wakidai viongozi hao wakuu waliwazungumzia ‘kama watoto wadogo’.
Kikao cha pamoja cha wabunge wa ODM na wale wa Kenya Kwanza kiligeuka uwanja wa zomazoma kwa Bw Odinga na Rais, mkutano huo ukiisha bila hata maafikiano kusomwa.
Bw Odinga alizomewa na wabunge ambao walieleza kukerwa na shinikizo zake kuwa wapokonywe Hazina ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NG-CDF).
Rais William Ruto naye hakusazwa, wabunge wakimkaba koo na kudai anawaandama kwa tuhuma za kupokea hongo ilhali wamekuwa wakikabiliwa na hali ngumu kutetea utendakazi duni wa serikali yake kwa raia.
Hasira zililipuka licha ya mkutano huo kutarajiwa kutumika kunogesha ushirikiano wa vyama vya UDA na ODM hasa kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.
Bw Odinga alikuwa akihutubu kuhusu jukumu la wabunge la kufuatilia utendakazi wa serikali na kutetea kaunti zipewe CDF, wabunge waliponung’unika na kumzomea licha ya kujitahidi kutoa ufafanuzi.
“Kazi ya bunge ni uwakilishi, kutunga sheria na kutathmini utendakazi. Hilo ni wazi. Bunge halifai kutekeleza, Bunge linafaa kutia kwenye mizani,” Raila akasema huku wabunge wakiingilia kati na kumvuruga.
Rais Ruto ambaye alikuwa ameketi chini pamoja na wote waliohudhuria, alionekana akiuelekeza mkono wake nyuma na kuashiri wabunge wasimzomee Bw Raila.
Bw Odinga aliyeonekana kukerwa na hatua ya wabunge hao, aliwaambia kuwa watakuwa na nafasi ya kusema kauli zao na kujibu msimamo wake.
“Ninaomba mnisikilize kisha mtakuwa na nafasi ya kujibu,” akasema Bw Raila akionekana kutikiswa.
Bw Raila aliwakera wabunge hao zaidi alipodai kuwa wao hupokea hongo kutoka kwa maafisa wa serikali ambao wanafika mbele yao ili waandike ripoti zinazowaondolea lawama kuhusu madai mbalimbali.
Aliposimama kuhutubu, Rais Ruto naye hakusazwa huku wabunge wakimtaka azungumzie madai yake ya kuwa wanapokea hongo aliyoyatoa akiwa Homa Bay wakati wa Kongamano la Ugatuzi.
Baadhi hata walimpigie kelele na kumwambia atahudumu muhula moja pekee wakipaza sauti na kusema ‘Wan Tam’ kauli ambayo imekuwa ikienezwa sana na vijana wasioridhishwa na uongozi wa Rais Ruto.
Wabunge hasa walimtaka ataje wale ambao amekuwa akisema walipokea hela hizo.
“Sitawataja na kuwaaibisha hapa, tutawakamata,” akasema Rais huku akifunguka moyo na kusema wao hupata pesa hizo kutoka kwa magavana.
“Niambieni unatoa wapi Sh150 milioni? Hizo ni pesa za kaunti. Wabunge walipokea hongo ya Sh10 milioni kupitisha Mswada wa Utakatishaji wa Pesa,” akaongeza Rais Ruto.
“Si mlipata pesa? Mnakusanya pesa kisha kugawana nyie watu wachache na kuharibu maadili ya bunge,” akasema akionekana pia kukabiliana na manung’uniko ya wabunge.
Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki alionekana kutambua ghadhabu za wabunge hao na kuwataka wasipuuze kile ambacho Rais na Bw Odinga wamefanyia nchi.
“Lazima tusherehekee uongozi wa kuridhisha wa wanasiasa hawa wawili. Viongozi vijana wanafaa wajifunze kutoka wanasiasa hawa kwa sababu kusimamia nchi si kazi rahisi,” akasema Profesa Kindiki.
“Kuna wanasiasa ambao wanakimbia hapa na pale na wakipewa nafasi hata siku moja kuendesha nchi, taifa litazama,” akasema Profesa Kindiki.
Baadhi ya wabunge ambao hawakutaka kunukuliwa walisema ni utovu wa maadili kuzomewa na Raila na Rais Ruto kama watoto wadogo ilhali wamekuwa wakitetea serikali kwa Wakenya.
“Hawatafaulu wakichukua huo mkondo wa kuwaandama wabunge na hatutakubali. Kama wanataka kubadilisha uongozi bunge waseme tu badala ya kutumia mianya na njia za mkato,” akasema mbunge mmoja aliyekataa kutajwa.
Mkutano wa jana uliishia kwa hasira wala mapendekezo yaliyoafikiwa hayakusomwa.
Mbunge mwengine naye aliipuuza taarifa iliyotolewa na UDA kuwa mkutano huo uliafikia utekelezaji wa Agenda Nne zilizotiwa saini kati ya chama hicho na ODM.
“Hatukuafikia chochote na mkutano huo uliisha vibaya walipoanza kutuvamiwa kuhusu hongo na CDF. Waseme ukweli kwa nini maafikiano hayakusomwa mkutanoni,” akasema mwengine ambaye pia hakutaka anukuliwe.
Wabunge ambao walikuwa karibu 100 walikataa mwaliko wa Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah wakunywe chai baada ya kuzomewa na Rais na Ruto huku wengi wakinungúnika wakiwa na hasira na kuingia kwenye magari yao yaliyoondoka kwa kasi.