Habari za Kitaifa

Wabunge wanaotishia kupiga kura kumtimua Linturi

April 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA JESSE CHENGE 

KUNDI la wabunge chini ya muungano wa Azimio la Umoja na wengine kutoka UDA, limetangaza nia kutaka kumwondoa afisini Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi, kutokana na skendo ya mbolea feki.

Wakiongozwa na Mbunge wa Bumula, Jack Wamboka, pamoja na Antony Kibagendi (Kitutu Chache), watunga sheria hayo wamesema taifa halitaendelea kuwa mateka ya utapeli hata katika sekta ya kilimo ambayo ndiyo nguzo na Kenya, kupitia usambazaji wa mbolea ghushi.

Wengine ambao wametishia kuwasilisha hoja ya kukosa imani na Waziri Linturi ni pamoja na Catherine Omanyo (Mwakilishi wa Wanawake, Busia), Caleb Amisi (Saboti), Mark Mwenje (Embakasi).

Gathoni Wamuchomba (Kithunguri), ambaye ni mbunge wa chama tawala cha UDA pia anaunga mkono ngoma ya kuondolewa kwa Bw Linturi iandaliwe.

Wabunge hao wameweka makataa ya hadi Jumanne (Aprili 16, 2024) kwa Rais William Ruto kumfuta kazi Waziri Linturi, la sivyo watawasilisha hoja ya kumshtaki.

Wamedai kuwa Rais amekuwa kimya huku wakulima wakiendelea kuteseka chini ya uongozi wa Linturi.

“Rais Ruto lazima achukue hatua na kumwondoa Linturi ofisini, la sivyo atatazamwa kama mshirika katika kashfa hii,” alidai Wamboka.

Omanyo alisema kuwa haiwezekani mbolea bandia kuuzwa kwa wakulima bila Rais kuwa na ufahamu.

Naye Mwenje alisisitiza kuwa wakati wa serikali ya Jubilee, ambapo Ruto alikuwa Naibu Rais, Mawaziri wawili ambao walishindwa kutekeleza majukumu yao walichujwa kazi.

“Rais wa zamani, Uhuru Kenyatta, alimfuta kazi Waziri wa Barabara Michael Kamau na Felix Kosgey wa Kilimo. Kwa nini Linturi anaonekana kuwa tofauti?” alitaka kujua Mwenje.

Mbunge huyo alielezea wasiwasi kuhusu mgawanyiko uliopo ndani ya Wizara ya Kilimo na alisisitiza kuwa suluhisho pekee ni kumwondoa Linturi kutoka wadhifa wake.

Wamboka alifichua kuwa wamekamilisha taratibu zote na ifikapo Jumanne watawasilisha hoja ya kumng’atua Waziri huyo.

“Hatuwezi kukubali Linturi kuharibu sekta ya kilimo,” alionya Wamboka.

Alielezea masikitiko yake kwamba Rais alikuwa anamlinda Linturi kwa gharama ya wakulima.

Naye Bi Wamuchomba alilaumu serikali kwa kile alichodai imesababisha wananchi kuteseka.

“Mpango wa Kenya Kwanza umeshindwa kulipa madaktari, umeshindwa kutoa fedha kufanikisha elimu bila malipo na badala yake wakulima wamebeba mzigo wa kodi kubwa,” alisema Wamuchomba.

Mbunge huyo wa UDA alisema serikali inapaswa kurejesha mpango wa Linda Mama ulioanzishwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.