Habari za Kitaifa

Wabunge waonywa dhidi ya kupitisha mswada unaoharamisha LGBTQ

April 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

HUKU Bunge la Kitaifa likirejelea vikao vyake Jumanne, Aprili 9, 2024 baada ya likizo, limeonywa dhidi ya kupitisha mswada unaolenga kuharamisha shughuli za ushoga (LGBTQ) nchini.

Mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu Fred Ogolla, anasema mswada huo, “Family Protection Bill, 2023” unaendeleza ubaguzi na utachangia Kenya kupoteza ufadhili wa kima cha Sh4.186 trilioni kutoka kwa asasi za kifedha za kimataifa.

Mswada huo umedhaminiwa na Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Opondo Kaluma ambaye ametaja ushoga katika “dhambi kubwa inayokwenda kinyume na maadili ya kitamaduni na kidini.”

“Suala la mahusiano ya kingono ya jinsia moja ni dhambi kulingana na mafundisho ya Biblia, Taifa na dini ya Kikristo. Hili ni suala la kimaadili bali sio la kisheria kwa hivyo hakupasi kupitishwa sheria ya kuharamisha LGBTQ na shughuli nyinginezo kuhusu mahusiano hayo,” Profesa Ogolla akaambia Taifa Dijitali, Aprili 8, 2024 kwenye mahojiano kwa njia ya simu.

Alisema mojawapo ya sababu zilizochangia kesi ya kupinga Sheria ya Fedha ya 2023 kuwasilishwa mahakamani ni kwamba iliendeleza ubaguzi haswa kuhusiana na sehemu iliyoanzisha utozaji ushuru wa nyumba.

“Vivyo hivyo, mswada huu uliodhaminiwa na Peter Kaluma unaendeleza ubaguzi dhidi ya kundi fulani la wanajamii na hivyo kuhujumu haki zao za kimsingi,” akasema Profesa Ogolla ambaye hata hivyo, aliweka wazi kuwa haungi mkono ushoga.

“Binafsi nachukulia ushoga kama dhambi lakini napinga kutengwa kwa mashoga bali wasaidiwe kupitia ushauri kutoka kwa viongozi wa kidini, washauri nasaha na wanasaikolojia,” akaeleza.

Alitoa wito kwa Bw Kaluma na wakili Charles Kanjama waliyesaidiana kuandaa mswada huo kuiga mfano wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis aliyeshauri Mapdre wa Kanisa hilo kutowatenga mashoga bali wawaombee.

“Papa Francis anatambua kuwa ushoga ni dhambi lakini wenye kutenda dhambi hiyo hawafai kutengwa bali wanafaa kuombewa na kushauriwa waasi mienendo hiyo,” Prof Ogolla akasema.

Alionya kuwa mashirika ya kimataifa ya kifedha kama vile Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Umoja wa Ulaya (EU) ambayo huipa Kenya misaada ya kufadhili bajeti na shughuli za kibinadamu yanaweza kuzima misaada hiyo ikiwa mswada wa Bw Kaluma utapitishwa.

“Wabunge wetu wasifanye Kenya kuiga mkondo wa nchi za Uganda na Ghana ambazo zilinyimwa ufadhili wa kimataifa baada ya kupitisha sheria kama hii dhidi ya LGBTQ. Nimepiga hesabu na kubaini kuwa Kenya itakosa jumla ya Sh4.186 trilioni kama msaada kutoka kwa wafadhili hawa ikiwa mswada huu utapitishwa na Rais William Ruto autie sahihi iwe sheria,” akaeleza Profesa Ogolla ambaye pia ni kiongozi wa Vuguvugu la Operation Linda Ugatuzi.

Amemtaka Rais kutotia saini mswada huo endapo utapishwa na wabunge.

Mswada huo unapiga marufuku mahusiano ya kingono ya jinsia moja, ndoa za jinsia moja na shughuli zozote za kuvumisha mahusiano kama haya, ikiwemo kuzifadhili.

Unapendekeza adhabu ya kifo au kifungo cha miaka 10 kwa watu watakaopatikana na hatia ya kushiriki mienendo hii.