Habari za Kitaifa

Wabunge wapinga madiwani kuanzishiwa pensheni: ‘Itakuwa mzigo kwa serikali’

Na SAMWEL OWINO August 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MSWADA unaolenga kuanzisha mpango wa pensheni kwa madiwani baada ya kustaafu, unakumbwa na pingamizi kali katika Bunge la Kitaifa huku wabunge wakielezea wasiwasi kuhusu gharama yake kwa mlipa-ushuru iwapo utapitishwa kuwa sheria.

Mswada wa Hazina ya Pensheni ya Mabunge ya Kaunti, 2024, unapendekeza kuanzishwa kwa mpango wa kustaafu wa madiwani na kuunda Hazina ya Pensheni ya Mabunge ya Kaunti kulipa au kutoa marupurupu ya kustaafu.

Mpango huo utakuwa wa kuchangia ambapo MCA atapokea malipo ya mara kwa mara kupitia pensheni kila mwezi, mapato ya kustaafu, au pensheni ya kiwango cha chini, kulingana na kanuni za Mamlaka ya Malipo ya Kustaafu (RBA).

Kulingana na Mswada huo kila MCA atachangia asilimia isiyopungua 7.5 ya mshahara wake wa pensheni kila mwezi.Serikali ya kaunti (kama mwajiri) itachangia asilimia isiyopungua 15 ya pensheni ya MCA huyo.

Hata hivyo, ripoti ya siri ya wataalamu wa sheria wa Bunge inaonya kwamba utekelezaji wa mswada huo utagharimu fedha nyingi za umma.

Ripoti hiyo inasema iwapo mswada huo utapitishwa, mabunge ya kaunti yatatakiwa kutenga fedha nyingi kutoka kwa mgao wao wa mapato ya kitaifa kuchangia mpango huu.

Hii itaathiri moja kwa moja miradi ya maendeleo, kwani fedha zaidi zitaelekezwa kwa pensheni badala ya miradi ya huduma kwa wananchi.

“Mswada huu unaweza kukwamisha miradi ya maendeleo kwa sababu ya mzigo mkubwa wa kifedha unaotokana na mchango wa lazima wa waajiri kwa kila MCA,” inasema ripoti hiyo.

TAFSIRI: BENSON MATHEKA