• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Wabunge warai serikali iwakabili wanaouza mbolea feki

Wabunge warai serikali iwakabili wanaouza mbolea feki

NA VITALIS KIMUTAI

BAADHI ya wabunge kutoka Rift Valley wametaka hatua kali ichukuliwe dhidi ya wafanyabiashara wakora ambao wanawauzia wakulima mbolea feki.

Wabunge Richard Yegon (Bomet Mashariki), Johanna Ng’eno (Emurua Dikirr), Richard Kilel (Bomet ya Kati) na Joseph Cherorot (Kipkelion Mashariki), walisema matumizi ya mbolea feki yatapunguza uzalishaji wa chakula na mimea kukosa kunawiri.

Kauli yao imekuja wakati ambapo Shirika linalotoa huduma ya ukaguzi wa mimea (Kephis) limeanza operesheni ya kuwanasa wafanyabiashara wanaowauzia wakulima mbolea feki.

Wabunge hao wa UDA wakiongea maeneo tofauti, walisema kuuzwa kwa mbolea feki ni njama ya kusambaratisha kilimo nchini ilhali ndicho kitega uchumi kwa taifa.

Walisema mbolea feki itapunguza uzalishaji. Hii, walisema, ni kinyume na mikakati ya Rais William Ruto kugeuza Kenya nchi inayojitosheleza kwa uzalishaji wa chakula.

“Ni vyema iwapo serikali itawakabili wafanyabiashara wakora ambao wana ujasiri na kiburi cha kusambaratisha mpango wa Rais. Serikali imekariri mara kadhaa kuwa inalenga kuinua kilimo ili kupunguza gharama ya kuagiza chakula nje ya nchi. Hilo halitawezekana wakulima wakiuziwa mbolea feki,” akasema Bw Yegon.

Chini ya mpango wa kuuza mbolea ya bei nafuu, serikali tayari imeagiza magunia milioni 12.5 huku pia ikitenga Sh10 bilioni kununua mbolea mwaka huu wa kifedha.

  • Tags

You can share this post!

Hii ndio siri ya kufaulu katika biashara

Polisi matatani kwa kudaiwa kuruhusu mauaji ya mshukiwa

T L