Habari za Kitaifa

Wacheni porojo kuhusu SHA, Wetang’ula aambia upinzani

Na BENSON MATHEKA October 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula amesifu mpango wa mageuzi ya huduma za afya kupitia Mamlaka ya Afya kwa Jamii (SHA), akisema ni mojawapo ya mafanikio makubwa ya serikali ya Rais William Ruto.

Akihutubu katika Shule ya Msingi ya Mukothima, eneobunge la Tharaka, wakati wa hafla ya kuwawezesha wanawake iliyoandaliwa na Mbunge George Murugara, Wetang’ula alisema SHA inalenga kumtumikia Mkenya wa kawaida kwa gharama nafuu na huduma bora.

“Kwa mara ya kwanza, tuna mfumo unaoweka afya ya wananchi mbele. SHA si porojo, ni suluhisho halisi,” alisema huku akishangiliwa na wakazi.

Wetang’ula pia alipuuza vikali upinzani, akisema viongozi wake wanaendeleza siasa za matusi, chuki na kejeli badala ya kutoa sera mbadala.

“Wanapoulizwa mpango wao, wanasema tu ‘Ruto lazima aende’. Hiyo si sera, ni kelele. Kenya haiwezi kuongozwa kwa hasira,” alisema.

Spika huyo alieleza kuwa serikali ya Ruto imeleta mabadiliko ya kweli katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba nafuu, miundombinu na kuimarika kwa uchumi ambapo thamani ya  shilingi ya Kenya imeimarika kutoka Sh160 hadi Sh128 kwa dola ya Amerika.

Aliwahimiza wananchi kumuunga mkono Rais Ruto kwa muhula wa pili, akimtaja Naibu Rais Prof Kithure Kindiki kama kiongozi mwenye nidhamu na mfano bora wa uongozi wa heshima.

Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah aliwahimiza vijana kujisajili kama wapiga kura, huku wabunge wengine wakisisitiza kuwa maendeleo yatazidi kushinda propaganda za upinzani.

Mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini, Japheth Nyakundi, aliwahimiza wakazi kumuunga mkono Prof Kindiki, huku Mbunge wa Taita Taveta, Victor Bwire, akisema: “Tutamchagua tena Rais Ruto 2027, na 2032 tutamuunga mkono Prof Kindiki.”

Wetang’ula aliahidi kuwa ziara hiyo ilikuwa mwanzo wa utekelezaji wa miradi zaidi ya kuwawezesha wananchi katika eneo hilo.