• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Wachukuzi wahofia mabogi mapya ya treni yanawalenga

Wachukuzi wahofia mabogi mapya ya treni yanawalenga

NA ANTHONY KITIMO

WASHIKADAU katika sekta ya usafiri wamehofia serikali inarudisha mfumo walioupinga wa kutumia reli ya kisasa (SGR) na ile ya zamani (MGR) kusafirisha mizigo kutoka bandari ya Mombasa hadi Malaba jambo ambalo litaathiri biashara zao.

Kuzinduliwa kwa mabogi 430 wiki hii, siku chache tu baada ya mabogi 50 mengine kuagizwa ili kutumika kusafirisha mizigo, wanadai ni njama fiche ya kurudisha amri ya kutumia reli ilikuongeza mapato ya shirika la reli nchini (KRC).

Kwa sasa, serikali imeongeza mabogi kutoka 1,600 hadi 1,900 ya SGR huku ya MGR ambayo inanuia kusafirisha mizigo kutoka Naivasha hadi Malaba kuongezeka kutoka mabogi 1,395 hadi 1,595 jambo ambalo limetia hofu washikadau katika sekta hiyo.

“Tulikutana na viongozi wa bandari nchini (KPA) na tukakubaliana kuhusu pendekezo la kutumia reli moja kwa moja kutoka bandarini lisitishwe kwa muda. Lakini kuletwa kwa mabogi zaidi kunaashiria nia ya serikali kuendelea na mpango huo,” alisema Bw Nasseb Mbarak, mwakilishi wa muungano wa kampuni za kusaga nafaka.Mwenyekiti wa muungano wa mawakala nchini (KIFWA).

Roy Mwanthi naye asema ni kinyume na ahadi ya serikali ya William Ruto kwamba angerudisha biashara za bandari kutoka Nairobi na Naivasha hadi Mombasa.

“Tunaomba Halmashauri ya bandari nchini (KPA) izingatie kupokea mizigo na kuacha shughuli za kusafirisha mizigo kwa wanaohusika. Ni kinyume cha sheria kutekeleza kazi ambazo si jukumu lao,” alisema Bw Mwanthi.

Washikadau katika sekta hiyo wanadai serikali inarudisha sheria walizozipinga wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ambapo wafanyabiashara walilazimishwa kubeba mizigo kutumia SGR.

Kulingana na waziri wa uchukuzi na barabara nchini Kipchumba Murkomen, serikali inanuia kusafirisha mizigo kutumia reli ilikupunguza msongamano bandarini na kupunguza kutegemea barabara.

Kwa kutumia mfumo huo, serikali inanuia kusafirisha mizigo tani milioni 11 kwa mwaka kutumia SGR hadi Naivasha kisha kutumia reli ya zamani hadi Malaba ili kupunguza muda wa kusafirisha mizigo kwa nchi zinazotumia bandari kama vile Uganda, Rwanda, Kongo na Sudan Kusini.

Hata hivyo, Katibu wa uchukuzi Mohamed Daghar wakati akizindua mabogi 430 wiki hii alisema kwa sasa bandari ya Mombasa ina zaidi ya mizigo tani 100,000 na vyuma zaidi ya tani elfu 45 ambazo zinatakiwa kusafirishwa na hivyo basi mabogi hayo yatasaidia kupunguza msongamano.

 

  • Tags

You can share this post!

Chifu adai polisi wanahujumu vita dhidi ya pombe haramu

Liverpool dhidi ya Man City, WanaArsenal wakiomba droo  

T L