Habari za Kitaifa

Wadau wataka Kenya ikumbatie maonyesho kuimarisha biashara

Na STANLEY NGOTHO January 6th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

Waonyeshaji wa bidhaa kutoka Kenya wanahimiza kuimarishwa kwa mwonekano wa sekta ya uzalishaji kupitia maonyesho ya biashara ya kikanda na ziara za waonyeshaji ili kujipatia nafasi bora ya kibiashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Sekta ya uzalishaji nchini Kenya, ambayo ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa taifa, inaendelea kukumbwa na changamoto nyingi katika kupanua uwepo wake katika masoko ya kikanda licha ya fursa zinazotolewa na EAC.

Dkt Solomon Kinyanjui, Mkurugenzi Mkuu wa Sols Inclination Ltd, anayejulikana kwa kuandaa maonyesho ya biashara ya ndani na kimataifa, ametoa changamoto  kwa Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda (MITI) kuimarisha ushiriki wa wazalishaji wa Kenya katika maonyesho ya biashara ya kikanda na ziara za waonyeshaji kote Afrika Mashariki.

Mtaalamu huyo wa maonyesho ya kimataifa alisema kuwa mwaka wa 2025 Kenya ilipoteza fursa kadhaa za biashara ya kimataifa kufuatia hatua za kubana matumizi zilizowekwa na serikali, ambazo zilipunguza bajeti ya maonyesho ya biashara katika Wizara ya Biashara na Viwanda. Hatua hiyo inadaiwa kuathiri vibaya kiwango cha mauzo ya nje ya nchi mwaka huo.

“Ushiriki wa Kenya katika maonyesho ya biashara ya kimataifa ulikuwa mdogo. Hali hii inahusishwa na sera za serikali zilizodhuru maonyesho ya biashara pamoja na changamoto nyingine za kibiashara,” alisema Dkt Kinyanjui.

Aidha, Dkt Kinyanjui alitaka Wizara ya Biashara na Viwanda kuwezesha ushiriki ulioratibiwa na wenye chapa madhubuti ili kusaidia viwanda vya Kenya kupata masoko mapya, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushindani wa viwanda.

“Kwa mujibu wa takwimu za KNBS za 2024, sekta ya uzalishaji huchangia takriban asilimia 7.6 ya Pato la Taifa (GDP), lakini uwezo wake wa kuuza bidhaa katika masoko ya kikanda bado ni mdogo ikilinganishwa na wapinzani kama Tanzania na Rwanda. Maonyesho ya biashara ya kikanda kama Uganda Trade Expo, Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) na Maonyesho ya Kigali (EXPO Rwanda) yanatoa fursa kubwa ambazo bado hazijatumiwa kikamilifu kwa ushirikiano wa kibiashara baina ya kampuni,” alibainisha.

Hata hivyo, inasemekana kuwa biashara ndogo na za kati (SMEs) kutoka Kenya hushindwa kushiriki kutokana na gharama kubwa za maonyesho, ukosefu wa uratibu wa pamoja na ufuatiliaji hafifu baada ya maonyesho.

“MITI inapaswa kuanzisha dawati la kitaifa la maonyesho na ukuzaji wa biashara ili kuratibu, kuwezesha na kufuatilia ushiriki wa Kenya katika maonyesho ya kikanda. Pia ishirkiane na Muungano wa Wazalishaji wa Kenya (KAM), KEPROBA na Brand Kenya kuandaa vibanda vya kitaifa chini ya bendera moja ya ‘Kenya Industrial Showcase’,” alisema. Aliongeza kuwa ni muhimu kuanzisha ruzuku za kusaidia SMEs kugharamia vibanda na usafirishaji, kujadiliana kuhusu ada nafuu za maonyesho na kurahisisha usimamizi wa mizigo.

Mbali na diplomasia ya viwanda kupitia balozi za Kenya katika miji mikuu ya EAC ili kuwezesha mikutano ya kibiashara na hafla za mitandao wakati wa maonyesho, Dkt Kinyanjui pia alisisitiza umuhimu wa kukuza mifumo ya thamani ya kikanda.

“Serikali itumie maonyesho ya biashara kubaini ushirikiano wa viwanda wa mipakani unaowaunganisha wazalishaji wa Kenya na wasambazaji na wasindikaji wa kikanda,” aliongeza.