Wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Moi wafokea pendekezo la kurejea kazini bila Sh10 bilioni wanazodai
MASAIBU yanayokumba Chujo Kikuu cha Moi hayataisha hivi karibuni baada ya wahadhiri na wafanyakazi wengine wanaogoma kuweka masharti magumu wanayotaka yatatimizwe kabla ya wao kurejea kazini.
Hii ni baada ya Katibu wa Elimu ya Juu Beatrice Inyanga kupakia kwenye mtandao wa X kile alichotaja kama ratiba ya shughuli zitakazopelekea kufunguliwa kwa chuo hicho.
Hii ni pamoja na mikutano ya mashauriano kati ya usimamizi wa chuo hicho na vyama vya kutetea masilahi ya wanahadhiri na wafanyakazi wasio wahadhiri.
Mikutano kati ya maafisa wa vyama vya UASU na KUSU, kwa upande mmoja na usimamizi wa chuo kikuu cha Moi, kwa upande mwingi umeratibiwa kufanyika kesho, Jumatano.
Mwongozo uliotolewa na Dkt Inyangala unabashiri kuwa makubaliano ya kurejea kazini yatatiwa saini Jumatano kisha Seneti ya chuo hicho iamuru kifunguliwe Alhamisi.
Nao wanafunzi walitarajiwa kuanza kurejea chuoni kuanzia Ijumaa ili shughuli za masomo zianze Jumatatu Novemba 11, 2024.
“Katiba wa Elimu ya Juu atakuwa katika Chuo Kikuu cha Moi Ijumaa Novemba 8, 2024 kuwakaribisha wanafunzi chuoni humo. Wanafunzi wasivunjike moyo,” akaandika.
Hata hivyo, viongozi wa UASU na KUSU wamemsuta Dkt Inyangala kwa kuharakisha mambo bila sababu wakishikilia kuwa sharti malipo ya malimbikizi ya mishahara yao ya kima cha Sh10 bilioni yatolewe.
“Tutarejea kazini tu baada ya usimamizi kutoa pesa hizo. Sharti watoa malipo hayo yote kwa awamu moja au watoe ratiba ya malipo itakayokubalika na wanachama wetu,” akasema Nyabuta Ojuki, Katibu wa Uasu, tawi la Chuo Kikuu cha Moi.
Maafisa wa KUSU waliunga mkono kauli hiyo, wakiitaka chuo hicho kuharakisha malipo hayo.
“Usimamizi wa chuo utoe mishahara yetu na iwasilishe makato husika kwa hazina mbalimbali za kushughulikia masilahi ya wanachama wetu. Baada ya malipo hayo kutolewa ndipo tutasitisha mgomo na kurejea kazini,” akasema Bob Odhiambo Ng’ura, Mwenyekiti wa KUSU, tawi la Chuo Kikuu cha Moi.