Wafanyakazi wa East Africa Portland wafunga kiwanda wakipinga uteuzi wa Ruto
WAFANYAKAZI wa Kampuni ya kutengeneza simiti ya East Africa Portland Cement (EAPCC), Jumatatu Desemba 23, 2024, walifunga lango kuu la kiwanda cha Athi River na kulemaza shughuli wakilalamikia uteuzi wa mkurugenzi mkuu mpya wakidai mchakato ulijawa na upendeleo.
Wafanyakazi hao walisitisha shughuli za kutengeneza simiti siku mbili baada ya Bw Bruno O Obodha kuteuliwa na Rais Ruto Ijumaa iliyopita kuchukua nafasi ya Bw Mohammed Osman Adan ambaye alikuwa akihudumu kama kaimu mkurugenzi.
Mnamo Jumatatu Desemba 23, 2024, baadhi ya wafanyikazi wanaopinga uteuzi huo mpya, walizima mashine na kuziba lango kuu la kiwanda kwa kutumia matingatinga. Kuzima mashine kunamaanisha kusimamisha uzalishaji.
Bw Obodha alitarajiwa katika kiwanda hicho Jumatatu asubuhi lakini baada ya mzozo huo hakufika.
Kwa siku nzima, hakuna lori lolote lililoruhusiwa kuingia au kuondoka kiwandani huku maafisa wa polisi wenye silaha kwa kawaida hutumwa kulinda kiwanda wakitazama bila msaada.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, wafanyakazi hao waliambia Taifa Leo kwamba hawana imani na mkurugenzi mkuu mteule huyo mpya wakisema kuna mgongano wa kimaslahi na kampuni hiyo na anakosa uwezo wa kiufundi unaohitajika kubadilisha kampuni na kuipa mwelekeo mzuri baada ya kupata hasara kwa miaka mingi.
“Kuhusika kwa Bw Obodha katika kampuni inayofanya biashara moja kwa moja na EAPC kupitia udhibiti wa ardhi kunaleta mgongano wa kimaslahi. Hii itajumuisha kufanya maamuzi na kuibua wasiwasi wa kimaadili kuhusu kutopendelea na uwazi unaohitajika kwa jukumu la Mkurugenzi Mkuu,” inasema sehemu ya taarifa kwa vyombo vya habari iliyosomwa na Bw Alex Muluwa, mfanyakazi.
Taarifa iliongeza: “Wakati wa mahojiano ya Novemba, kaimu mkurugenzi mkuu Mohammed Aden aliibuka bora kwa alama za juu.”
Taifa Leo ilipata vidokezi za mkutano maalum wa bodi ya wakurugenzi uliofanyika katika afisi ya kampuni hiyo katika Taj towers mnamo Ijumaa Novemba 22 2024 zikionyesha Bw Mohammed Osman Adan aliibuka bora kwa kupata asilimia 88.15 Bruno O Obodha aliibuka wa pili kwa kupata asilimia 64 akifuatiwa kwa karibu na Dkt Justa Mwangi aliyepata asilimia 63.86.
Wafanyikazi hao wanamtaka Rais Ruto na Mkuu wa Utumishi wa Umma kuteua anayestahili kwa wadhifa huo wakiapa kuendelea kulemaza shughuli hadi malalamishi yao yatakaposikizwa.
Bw Mohamed alichaguliwa na bodi, kama kaimu mnamo Machi 26 2024 kuchukua nafasi ya Bw Oliver Kirubai. Bw Mohammed amekuwa akifanya kazi Portland na kupanda cheo hadi mkuu wa fedha katika miaka mitatu iliyopita.