Wafanyakazi wa hospitali kulipwa nusu ya mshahara SHA ikikwama na pesa
WAFANYAKAZI wa kandarasi katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega (KCGH) watalipwa nusu ya mshahara wao kuanzia mwezi Agosti, kutokana na uhaba mkubwa wa fedha unaoikumba hospitali hiyo.
Hali hii inatokana na kucheleweshwa kwa malipo kutoka kwa Mamlaka ya Bima ya Afya ya Jamii (SHA), ambayo haijatoa fedha kwa huduma zilizotolewa na hospitali hiyo kwa miezi miwili mfululizo.
Katika barua rasmi kwa wafanyakazi, usimamizi wa hospitali hiyo ulisema kuwa mapato ya kila mwezi yameshuka kwa zaidi ya nusu ikilinganishwa na hapo awali.
“Kwa kuzingatia hali hii, tumekubaliana kwamba iwapo fedha hazitatumwa kufikia mwisho wa mwezi, idara ya fedha italipa nusu ya mshahara, na salio litakulipwa SHA itakapotoa pesa,” alisema Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Afya katika hospitali hiyo, Bw Hillary Kiverenge.
Aliongeza kuwa ucheleweshaji huo umezua mgogoro mkubwa wa kifedha, hali inayosababisha usumbufu mkubwa katika utoaji huduma.
Hospitali ya Mukumu pia haijapokea fedha kutoka SHA kwa miezi ya Julai na Agosti. Askofu Joseph Obanyi wa Kanisa Katoliki alielezea hofu kuwa hospitali hiyo inaweza kufungwa kama ilivyotokea kwa Hospitali ya St Mary’s, Mumias.
“Hali si shwari Mukumu. Nimejulishwa kuwa hawajapokea fedha kwa miezi miwili sasa,” alisema Askofu Obanyi.
Taasisi nyingi, hasa zinazomilikiwa na makanisa, zinakabiliwa na hatari ya kufungwa kutokana na kucheleweshwa kwa malipo halali kutoka SHA.
Ingawa baadhi ya hospitali zimetuhumiwa kuwasilisha habari feki, changamoto kuu inayozikumba ni kutolipwa malipo halali, hali inayotishia uendelevu wa Huduma ya Afya kwa Wote nchini Kenya.