Wafanyakazi wa JKIA waliositisha mgomo kuchunguza dili ya Adani warejea na kauli: ‘Ni sumu’
WAFANYAKAZI wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) wamekataa mpango wa serrkali wa kukodisha uwanja huo kwa kampuni ya Adani kutoka India wakisema ni sumu.
Wafanyakazi hao, wanachama wa chama cha kutetea wafanyakazi wa viwanja vya ndege Kenya (KAWU) ambao walikubali kusitisha mgomo wao ulioathiri shughuli katika viwanja vya ndege mnamo Septemba 11 walisema tangu wakati huo wamechanganua stakabadhi kuhusu mpango huo na kugundua kuwa makubaliano hayo ni sumu.
Katibu Mkuu wa KAWU, Bw Moss Ndiema alisema kwamba maafisa wa chama watakutana na wenzao wa serikali wiki ijayo kueleza msimamo wao na kisha watatangaza hatua inayofuata.
“Kama chama tumepitia stakabadhi walizotupa na tunaeleza kuwa ni mbaya. Hatutaki Adani isimamie uwanja wetu wa ndege na tutaweka wazi hilo kwa serikali wakati wa mkutano wetu wiki ijayo,” Bw Ndiema aliambia Taifa Jumapili mnamo Ijumaa Septemba 27.
Maafisa wa chama hicho walitia saini mkataba wa kurejea kazini mnamo Septemba 11 kufuatia mgomo wao uliolemaza shughuli katika viwanja tofauti vya ndege nchini.
Mgomo huo ulisababisha hasara ya takriban Sh80 milioni za mapato kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Airways Allan Kilavuka.
Muafaka wa kurejea kazini ulitoa muda wa siku 10 kwa maafisa wa vyama vya wafanyakazi kupitia pendekezo lililoanzishwa na Adani kabla ya kufanya uamuzi huo.
Maafisa wa Kawu wanapinga kile wanachosema kuwa ni masharti katika mkataba wa Adani ambayo yatawafanya kupoteza nafasi zao za ajira.
Pia wanataka maafisa wakuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (KAA) kujiuzulu kwa kujihusisha na mpango huo.
Kipindi cha makubaliano hayo pia kitadumu kwa miaka 30 kutoka tarehe ya kuanza kwa mpango huo ikiwa pendekezo litakubaliwa.
Katika kipindi hiki, Adani itakarabati uwanja huo wa ndege.
Adani pia inapendekeza kwamba KAA iagizwe kuongeza ada za uwanja wa ndege kulingana na tathmini ambayo itafanya.
“Mfadhili atachukua ndani ya siku 90 hatua madhubuti za kukarabati Uwanja wa Ndege kama inavyopendekezwa. Ada zitaamuliwa kulingana na mfumo utakaokubaliwa na kubainishwa katika Makubaliano. Msingi wa kubainisha gharama za uwanja wa ndege ni kama ifuatavyo: asilimia 100 ya biashara ya anga, asilimia 100 ya biashara ya maegesho ya magari na asilimia 30 ya mapato kabla ya riba na kodi,” inasema sehemu ya mpango huo.
Bw Ndiema alipuuzilia mbali mpango huo akiteta kuwa hakuna mfanyakazi yeyote aliyehusika katika shughuli hiyo na kwamba walifahamu kuhusu mpango huo kupitia mitandao ya kijamii.
‘Haijalishi kama ni kukodisha au kuuza. Nimesikia wakisema hawauzi wanakodisha. Ukweli wa mambo ni kwamba ifikapo mwisho wa miaka 30, hakuna hata mmoja wa wafanyakazi hawa atakuwa hapa. Inasikitisha sana kwamba usimamizi wa KAA umekuwa kimya kuhusu hili,” Bw Ndiema alisema.