Habari za Kitaifa

Wafugaji, Maimamu nao wapinga mpango wa chanjo ya mifugo kitaifa

Na STANLEY NGOTHO, SHABAN MAKOKHA December 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BAADHI ya wafugaji katika kaunti ya Kajiado wameapa kutoshiriki katika shughuli ijayo ya utoaji chanjo kwa mifugo huku viongozi wa kiislamu wakitaka serikali kufanya mazungumzo na raia kuhusu suala hilo.

Serikali ya Kitaifa kupitia Idara ya Ustawi wa Mifugo imetangaza kuanzisha mpango wa utoaji chanjo kwa ng’ombe 22 milioni kuzuia ugonjwa wa miguu na midomo (FMD) na kondoo na mbuzi 50 milioni dhidi ya ugonjwa wa Pes des Petits (PDP).

Rais William Ruto amekuwa akitetea mpango huo akishikilia kuwa chanjo hiyo ni salama na imetengenezwa humu nchini.

Hata hivyo, viongozi wa upinzani wakiongozwa na Kalonzo Musyoka wamepinga shughuli hiyo ya utoaji chanjo kwa mifugo wakidai italeta madhara kwa mifugo.

Wamewaonya wafugaji dhidi ya kuwasilisha mifugo wao kuchanjwa wakisema shughuli hiyo imedhaminiwa na taasis za kigeni za kufanya utafiti wa dawa za mifugo zenye chembechembe za kubadilisha maumbile ya mifugo.

Wakiongea jana katika wadi ya Poka Kenyawa, Kaunti Ndogo ya Kajiado Mashariki, wakitoa baraka kwa Wamoran 4,000, wafugaji wengine walisema hawataruhusu mifugo wao kupewa chanjo.

“Tuko na mpango wetu wa kutoa chanjo kwa mifugo wetu. Tulitaraji serikali kuingilia kati na kutusaidia wakati wa msimu wa mvua lakini haikufanya hivyo. Tuko na maswali mengi ambayo hayajajibiwa kuhusu mpango huo wa utoaji chanjo,” akasema Bw Sekento Keleu.

Wafugaji walisema hawafai kulazimishwa na serikali kuruhusu mifugo wao wapewe chanjo ilhali serikali huwa haifanyi lolote kuhusiana na changomoto zingine zinazowazonga.

“Changamoto kubwa inayotukumba sasa ni mmea inaojulikana kama Ipmea. Mmea huo unaenea kwa kasi na hivyo unadidimisha lishe ya mifugo. Serikali ijue hatutalazimishwa kuwapeleka mifugo wetu wapewe chanjo,” akasema Ben Moloma ambaye ni mfugaji.