Habari za Kitaifa

Wafugaji waapa kususia chanjo ya mifugo Januari

Na MWANGI NDIRANGU December 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya wafugaji kutoka kaskazini mwa Kenya wanapinga chanjo ya mifugo inayopangwa kuanza Januari 2025 hadi serikali itakapotoa taarifa kamili kuhusu zoezi hilo.

Katika barua kwa Katibu katika wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Bw Abdulhakim Sheikh na Omar Maalim ambao ni wafugaji, wametoa matakwa kama vile kufichuliwa kwa jina na aina ya chanjo itakayotumika, muundo wake wa kemikali, faida na hatari kwa wafugaji na watumiaji.

Barua hiyo iliandikwa kupitia wakili wao Bw Eric Wachana wa Dahir, Affey and Associates Advocates LLP.

Nchi nzima, chanjo hiyo inatarajiwa kutolewa kwa ng’ombe milioni 20 dhidi ya Ugonjwa wa Miguu na Midomo (Foot and Mouth Disease) na kondoo na mbuzi milioni 50 dhidi ya Peste des Petits Ruminants (PPR).

Akiwa katika ziara ya Wajir mapema wiki hii wakati wa kongamano la wafugaji, Rais William Ruto alionya wanaopinga chanjo hiyo akisema kuwa kuikubali kutafanya nyama ya ng’ombe na kondoo nchini kukubalika katika soko la kimataifa.

Kabla ya mkutano huo, Rais Ruto alifanya mkutano na viongozi wa United Democracy Movement (UDM) chama kikuu cha kisiasa Kaskazini Mashariki mwa Kenya, ambapo waliahidi kuunga mkono mpango huo.

Lakini wafugaji hao wanadai kuwa jambo hilo linakiuka Katiba kwa kuwa wafugaji walio wengi hawakushirikishwa moja kwa moja.

Kumekuwa na madai kuwa chanjo hiyo kwa wingi inafadhiliwa na Wakfu wa Bill Gates ili kupunguza uzalishaji wa methane miongoni mwa mifugo nchini.

Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, pia amewataka wafugaji kutokubali chanjo hiyo, akiteta kuwa zoezi hilo linalenga kubadilisha maumbile ya mifugo ya asili na halihusiani na udhibiti wa magonjwa.

Mabw Sheikh na Maalim wanataka wafadhili halisi wa kampeni hio ya chanjo kuwekwa hadharani, ikiwa ni pamoja na wito wao wa kujihusisha nchini Kenya.

“Tunatoa wito kwa wizara kuweka hadharani faida ya muda mrefu itakavyozidi gharama inayotarajiwa ya chanjo ya mara kwa mara kama matokeo ili kuzuia uzalishaji wa methane duniani,” sehemu ya barua iliyowasilishwa kwa Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo inaeleza.

Pia, wanataka ripoti ya kina kuhusu lini sampuli za magonjwa zilikusanywa na kupelekwa kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi na utafiti kufanywa ili kufikia lengo la mwisho la chanjo ya mifugo.

Bw Sheikh na Bw Maalim wanataka majibu ndani ya siku saba.

Lakini Waziri wa Kilimo na Mifugo Andrew Karanja amewataka Wakenya kupuuza kile alichokitaja kuwa propaganda zinazoenezwa na wapinzani.