Wageni wanaozuru Pwani msimu huu wa sherehe watakiwa kutii masharti baharini
WAGENI wanaozuru maeneo ya Pwani kwa ajili ya likizo za Desemba wametakiwa kufuata masharti ya kiusalama ufukweni ili kuepusha majanga.
Wakuu wa usalama wamesisitiza hitaji la kila mmoja kuheshimu kanuni ya kuondoka baharini ifikapo saa kumi na mbili jioni, ambayo huwa ni hatua ya kudhibiti visa vya ukosefu wa usalama na watu kuzama majini.
Katika Kaunti ya Kilifi, Kamishna wa Kaunti, Bw David Wanyonyi, alionya kuwa, mawimbi ya bahari huwa makali zaidi na yasiyotabirika wakati wa usiku, hali inayowaweka hatarini watu wanaotembelea fukwe.
Aliongeza kuwa, kufungwa kwa fukwe mapema kutasaidia pia kuwalinda wakazi dhidi ya vitendo vya uhalifu ambavyo hutokea kutokana na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Huko Mombasa, Kamishna wa Kaunti, Mohamed Noor, alisema kikosi cha Shirika la Kuhifadhi Wanyamapori nchini (KWS) kimetumwa kusaidia Polisi wa Utalii na Machifu ili kuhakikisha usalama wa watu wanaotembelea fukwe.
“Saa kumi na mbili jioni, tutapiga filimbi kuhakikisha waogeleaji wote wanatoka ufukweni. Hatutaki mtu yeyote azame baharini au kujeruhiwa. Tumezielekeza pia hoteli kuhakikisha zina waokoaji wa majini, ili kuhakikisha hakuna anayefariki au kujeruhiwa kwenye mabwawa ya kuogelea,” akasema Bw Noor.
Vilevile, Bw Noor alisema usalama umeimarishwa katika maeneo yote ya Mombasa, ambayo inashuhudia ongezeko la watalii wa ndani na wa kimataifa.
Kamishna huyo aliwapongeza maafisa wa polisi kwa kuwakamata washukiwa 36 wa uhalifu katika Kaunti Ndogo ya Kisauni mapema Ijumaa asubuhi.
“Tutaendelea kukaza kamba ili kuhakikisha hakuna mtu atakayejitokeza kuwahangaisha watu hapa Mombasa, si wageni pekee bali hata wakazi,” alihakikisha.
Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, aliitaka serikali ya kitaifa kuharakisha upanuzi wa barabara ya Mombasa–Malindi na Uwanja wa Ndege wa Malindi ili kuvutia watalii zaidi katika kaunti hiyo.
“Mwaka jana pekee, Kilifi ilipokea zaidi ya watalii 500,000 wa ndani na wa kimataifa, idadi inayozidi wakazi wa miji ya Malindi na Kilifi. Hili ni ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na idadi ya watalii waliorekodiwa mwaka uliotangulia,” alisema.
Aliongeza kuwa, kaunti hiyo inaibuka kama kitovu bora cha utalii wa mikutano, na asilimia 40 ya watalii waliotembelea kaunti hiyo walikuja kwa ajili ya mikutano.
Wote walikuwa wakizungumza wakati wa sherehe za Jamhuri katika kaunti zao.
Kwingineko, Kamanda wa Polisi wa Trafiki eneo la Pwani, Bw George Kashimiri, alisema idadi ya maafisa wa trafiki imeongezwa barabarani ili kuimarisha utekelezaji wa sheria.
Alisema alama za barabarani zinazoonyesha kiwango cha mwendo kinachoruhusiwa zimeekwa jijini Mombasa, na yeyote atakayepitisha viwango vinavyohitajika atakamatwa.
“Sheria hii inawahusu madereva wa magari yote. Kwa kuwa idadi ya wageni inaongezeka, tumepeleka maafisa wa ziada. Katika maeneo yenye taa za trafiki tumepunguza idadi ya polisi na kuwapeleka katika maeneo yasiyo na taa. Tuna maafisa wa kutosha kusimamia Mombasa nzima. Pia tumeanza kutumia kifaa cha kupima kiwango cha ulevi wa pombe (Alco-blow) na tutaendelea nacho katika msimu wote wa sherehe,” alieleza.
Afisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama na Uchukuzi (NTSA), Bw Douglas Nyagwoka, alisema wiki iliyopita, madereva 23 wa mabasi ya kampuni moja Mombasa walisimamishwa kazi kwa kuendesha kwa kasi, na vifaa vyao vya kudhibiti mwendo vilisaidia maafisa husika kuwafuatilia.
“Kampeni hii itasaidia pakubwa. Magari yasiyo na vifaa vya kudhibiti mwendo huwa na athari kubwa zaidi yanapopata ajali. Pia tunafanya kazi na polisi wa trafiki kukabiliana na mwendo kasi katika eneo la Dongo Kundu,” akasema.
Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Matatu Salim Bates, aliwataka waendeshaji wa vyombo vya usafiri wa umma kuwa waangalifu na kuwasihi wasimamizi wa sekta hiyo kuimarisha usimamizi.