Wahadhiri wa Vyuo Vikuu 37 nchini wavuruga masomo kwa mgomo
HALI ya kutoaminiana kati ya wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma na serikali imechangia wahadhiri hao kugoma licha serikali kudai imetoa Sh2.5 bilioni za kulipia malimbikizi ya mishahara yao.
Taarifa ya Waziri wa Elimu Migos Ogamba jana, kutangaza kutolewa kwa pesa hizo ilipuuziliwa mbali na wahadhiri hao wakidai ililenga kuwachezea shere.
Mgomo huo uliotishwa na Chama cha Kutetea Masilahi ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU) ilianza jana huku maafisa wake katika vyuo mbalimbali wakiwaongoza wenzao kususia kazi.
“Tulitoa ilani ya mgomo siku saba zilizopita baada ya kusubiri kwa miezi mitatu bila kulipwa. Mbona mtu asubiri hadi baada ya mgomo kuanza ndiposa anaomba muda wa wiki mbili kabla ya kutulipa. Hizo ni hadaa ambazo hatutakubali,” akasema Katibu wa UASU tawi la Chuo Kikuu cha Nairobi Maloba Wekesa.
Alisema kuwa serikali ya Kenya Kwanza ilipoingia afisini iliahidi kuheshimu makubaliano kuhusu mishahara (CBAs) bila kulechewa, lakini sasa imetenda kinyume.
Wahadhiri wanaitaka serikali kutokma Sh2.73 bilioni kutoka kwa Awamu ya Pili ya CBA ya 2021-2025 ambazo zilipasa kulipwa Julai mwaka huu.
Pia wanataka walipwe Sh7.9 bilioni zilizosalia kutoka CBA ya 2017-2021 pamoja na majadiliano na kupitishwa kwa CBA ya 2025-2029.
Kwa mfano licha ya UASU kuwasilisha mapendekezo yao kuhusu CBA ya 2021-2025 kwa wakati, ilitiwa saini mnamo Novemba 23, 2024 ambapo Serikali iliahidi kulipa kwa awamu.
Awamu ya kwanza ya Sh3.4 bilioni zilipwa Januari 2025, awamu ya pili ya Sh2.73 bilioni zilipasa kulipwa Julai ilhali pesa za awamu ya tatu zilipasa kutolewa mnamo Septemba, mwaka huu.
“Tumechoshwa na ahadi tasa na tutaendelea na mgomo hadi tulipwe pesa hizo. Hiyo ndio lugha ya kipekee ambayo serikali inasikia,” akasema Dkt Wekesa.
Waziri Ogamba kwenye taarifa yake jana alisema serikali imejitolea kulipa pesa zote ilizopasa kulipa iliyokubaliwa katika mpango wa kurejea kazini.
Chama cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) na Chama cha Wafanyakazi wa Hoteli, Taasisi za Masomo na Hospitali (Kudheia) pia vimeungana na UASU kulemaza masomo katika vyuo 37 vya umma na vyuo vishirikishi.
“Tumeitisha mgomo huu kwa sababu serikali imefeli kutulipa. Kile ambacho nilipokea jana ni barua. Wahadhiri hawali barua,” akasema Katibu Mkuu wa UASU Dkt Constantine Wasonga, alipozindua mgomo huo katika Chuo Kikuu Maseno